SOMO 1
2 Samueli 7:1—5, 8b—12, 14a, 16
Hapo mfalme Daudi alipokuwa katika nyumba yake, na Bwana akiwa amemstarehesha, asibughudhiwe na adui zake waliomzunguka pande zote, mfalme akamwambia Nathani nabii, "Tazama, mimi ninakaa katika nyumba ya mierezi, na sanduku la Bwana linakaa katika hema!" Nathani akamjibu mfalme, "Haya, nenda ukafanye yote yaliyomo moyoni mwako, maana Bwana yu pamoja nawe." Lakini usiku huo huo neno la Bwana likamjia Nathani kusema: Nenda ukamwambie mtumishi wangu Daudi, Bwana asema hivi: Je, wewe utanijengea nyumba, nikae ndani yake? Mimi nalikutwaa katika kazi ya kuwalisha na kuwaandama kondoo ili uwe mkuu juu ya watu wangu Israeli; nimekuwa pamoja nawe popote ulipokwenda na nimewaondosha maadui zako wote mbele yako. Nami nitakufanyia jina kuu, kama jina la wakuu waliopo duniani. Nami nitawawekea mahali watu wangu Israeli, nitawapanda wapate kukaa mahali pao wenyewe, wasiweze kuondolewa tena, wala wana wa uovu hawatawasumbua tena, kama hapo zamani, tangu nilipowaweka waamuzi juu ya Israeli watu wangu. Nami nitakustarehesha mbele ya adui zako wote. Tena, Bwana anakufunulia kuwa atakujengea nyumba. Na siku zako zitakapotimia, nawe umejipumzisha na baba zako, nitamwinua mzao wako, baada yako atokaye viunoni mwako, nami nitauimarisha ufalme wake. Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu. Nayo nyumba yako na ufalme wako vitadumu milele mbele yangu, na kiti chako kitakaa imara milele.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 89:2—3, 4—5, 27 na 29
W. Fadhili za Bwana nitaziimba milele.
Fadhili za Bwana nitaziimba milele,
kwa kinywa changu nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako.
Maana ulisema: Wema wangu wadumu milele;
uaminifu wangu umesimikwa katika mbingu. K.
Nimefunga agano na mteule wangu;
nimemwapia Daudi, mtumishi wangu,
nitawasimika wazao wako hata milele,
nitaimarisha kiti cha ufalme wako kwa vizazi vyote. K.
Yeye ataniita, 'Wewe ni Baba yangu,
Mungu wangu na mwamba wa wokovu wangu!'
Nitamhifadhia fadhili zangu hata milele,
na agano langu kwake litadumu imara milele. K.
SOMO 2
Warumi 16:25—27
Ndugu zangu: Asifiwe mwenye enzi ya kuwaimarisha ninyi kadiri ya Injili yangu na tangazo la Yesu Kristo, pia kadiri ya ufunuo wa fumbo lile lililofichika tangu karne ya milele. Sasa lakini limefunuliwa kwa njia ya Maandiko ya manabii kama Mungu wa milele alivyotaka ili kuwaongoza mataifa yote wapate kuitii imani. Mungu mmoja mwenye hekima aheshimiwe na kusifiwa kwa njia ya Yesu Kristo, milele na milele. Amina.
Neno la Bwana.
SHANGILIO LA INJILI
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Tazama mimi ni mtumishi wa Bwana, nitendewe ulivyonena.
W. Aleluya.
INJILI
Luka 1:26—38
Wakati ule: Malaika Gabrieli alitumwa na Mungu aende katika mji wa Galilaya uitwao Nazareti, kwa mwanamwali bikira, mchumba wa mtu, jina lake Yosefu, wa nyumba ya Daudi, na jina la huyo bikira lilikuwa Maria. Na malaika akaingia kwake, akasema, "Salamu, uliyejaa neema! Bwana yu nawe." Naye akashtuka kwa sababu ya maneno hayo, na akawaza maana ya maamkio hayo. Malaika akamwambia, "Usiogope, Maria, kwa maana umebarikiwa na Mungu. Tazama, utachukua mimba na kumzaa mwana, na utampa jina Yesu. Huyo atakuwa mkubwa na kuitwa Mwana wa Aliye Juu na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi baba yake, ataitawala nyumba ya Yakobo hata milele, na utawala wake hautakuwa na mwisho." Maria akamwambia malaika, "Litakuwaje neno hili maana sijui mume?" Malaika akamjibu akisema, "Roho Mtakatifu atakushukia, na nguvu ya yule Aliye Juu itakufunika kwa kivuli chake. Kwa hiyo kitakatifu kitakachozaliwa kitaitwa Mwana wa Mungu. Hata jamaa yako Elizabeti amepata mimba ya mtoto mwanaume katika uzee wake; na huu ni mwezi wake sita kwa yeye aliyeitwa tasa; kwa maana hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu." Maria akasema, "Tazama, mimi ni mtumishi wa Bwana, nitendewe ulivyonena." Kisha malaika akamwacha, akaenda zake.
Injili ya Bwana.