SOMO 1
Malaki 3:1—4, 23—24a
Tazameni, namtuma mjumbe wangu, naye ataitengeneza njia mbele yangu. Atafika ghafla katika hekalu lake Bwana mnayemtaka, ujumbe wa agano mnayemtamani. Tazameni: anakuja, asema Bwana wa majeshi. Nani awezaye kuvumilia siku ya kuja kwake, na kusimama siku atakapotokea? Maana yeye ni kama moto wa mfua chuma, na kama sabuni ya mfua nguo. Basi ataketi akiyeyusha na kusafisha, atawasafisha wana wa Lawi na kuwatakasa, kama vile dhahabu na fedha, nao watamtolea Bwana matoleo jinsi inavyofaa. Nayo matoleo ya Yuda na Yerusalemu yatampendeza Bwana, kama vile siku za kale, na kama miaka ya zamani. Tazama, mimi nitamtuma kwenu Eliya Nabii kabla siku ya hukumu ya Bwana haijafika, siku kubwa ya kutisha. Naye ataigeuza mioyo ya baba iwaelekee wana, na mioyo ya wana iwaelekee baba, ili nisije nikaipiga nchi kwa maapizo.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 25:4—5ab, 8—9, 10 na 14
K. Inueni vichwa vyenu,
kwa maana ukombozi wenu unakaribia.
Ee BWANA, unionyeshe njia zako, / unijulishe mapito yako.
Uniongoze katika uaminifu wako, unifundishe,
maana wewe ndiwe Mungu mwokozi wangu. K.
Bwana ni mwema, tena mwenye haki,
kwa hiyo huwajulisha wakosefu njia zake.
Huwaongoza wanyenyekevu katika haki,
na kuwafundisha njia yake. K.
Mapito yote ya Bwana ni uaminifu na kweli
kwa wale washikao agano na amri zake.
Siri ya Bwana iko kwao wamchao, / naye huwajulisha agano lake. K.
SHANGILIO LA INJILI
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Njoo, ewe Mfalme wa mataifa na jiwe la msingi wa Kanisa! Uje na umwokoe mwanadamu ambaye ulimwumba kutoka katika udongo wa dunia.
W. Aleluya.
INJILI
Luka 1:57—66
Muda ulipotimia Elizabeti kujifungua, alimzaa mtoto mwanaume. Jirani na jamaa zake wakasikia ya kuwa Bwana amemzidishia huruma yake, wakafurahi pamoja naye. Basi, siku ya nane wakaja kumtahiri mtoto, na kumpa jina la baba yake Zakaria, lakini mama yake akawaambia, "La, sivyo. Ataitwa Yohane." Lakini wakamwambia, "Hakuna mtu katika jamaa zako aitwaye jina hilo." Wakamwuliza baba yake kwa ishara atakavyo kumwita. Akaomba kibao, akaandika, "Jina lake ni Yohane," na wote wakashangaa. Papo hapo akafunguliwa kinywa na ulimi, akanena na kumsifu Mungu. Hofu ikawashika jirani zao wote, na habari hizo zikavuma pote sehemu ya milimani huko Yudea. Wote waliozisikia wakaziweka mioyoni mwao, wakisema, "Je, mtoto huyu atakuwaje?" Kwa maana mkono wa Bwana umekuwa pamoja naye.
Injili ya Bwana.