SOMO 1
1 Samueli 1:24—28
Siku zile, [Hana] alipokwisha kumwachisha Samueli maziwa, alimchukua pamoja naye, na ng'ombe dume wa miaka mitatu, na efa moja ya unga, na chupa ya divai, akamleta katika hekalu la Bwana huko Shilo. Baada ya baba yake kumchinja na kumtolea sadaka yule ng'ombe dume, walimleta mtoto kwa Eli, na Hana mama yake akamwendea Eli, na kusema, "Samahani bwana, kama iishivyo roho yako, mimi ndimi yule mwanamke niliyesimama karibu nawe hapa, nikimwomba Bwana. Nilimwomba nimpate mtoto huyu, naye Bwana alisikiliza maombi yangu. Sasa nami pia, ninampa Bwana mtoto huyu; Akamwacha mtoto pale na kuondoka.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
1 SAMUELI 2:4—5, 6—7, 8ab, cd (K. 1a)
K. Moyo wangu wamshangilia Bwana, Mwokozi wangu.
Moyo wangu unamshangilia Bwana,
na pembe yangu imetukuka katika Mungu wangu.
Kinywa changu kimepanuka juu ya adui zangu,
kwa maana naufurahia wokovu wako. K.
Upinde wa mashujaa umevunjika,
bali walio dhaifu wamefungiwa nguvu.
Walioshiba wamejikodisha ili kupata chakula,
na hao waliokuwa na njaa wamepata raha.
Mwanamke tasa amezaa watoto saba,
naye mama wa wana wengi amefifia. K.
Ndiye Bwana anayeua, na anayehuisha,
hushusha hata kuzimu, tena huleta juu.
Bwana hufukarisha mtu naye hutajirisha,
hushusha chini, tena huinua juu. K.
Humwinua mnyonge kutoka mavumbini,
humpandisha mhitaji kutoka jaani,
ili awaketishe pamoja na wakuu,
wakakirithi kiti cha enzi cha utukufu. K.
SHANGILIO LA INJILI
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Njoo, ewe Mfalme wa mataifa na jiwe kuu la pembeni la kanisa!
Uje na umwokoe mwanadamu ambaye ulimwumba kutoka katika udongo wa dunia.
W. Aleluya.
INJILI
Luka 1:46—56
Siku ile: Maria alisema: "Moyo wangu wamtukuza Bwana; na roho yangu imeshangilia katika Mungu, Mkombozi wangu. Kwa kuwa ameangalia unyonge wa mtumishi wake; tazama, toka sasa vizazi vyote wataniita mwenye heri. Kwa maana amenitendea makubwa Aliye Mwenyezi, na jina lake ni takatifu. Na huruma yake ipo toka kizazi hata kizazi kwa wale wenye kumcha. Ameonyesha enzi kwa mkono wake, amewatawanya wenye kiburi mioyoni mwao. Amewaondosha wenye enzi katika kiti, akawakuza wanyonge. Wenye njaa amewashibisha mema; matajiri amewarudisha mikono mitupu. Amemsaidia Israeli, mtumishi wake, akiikumbuka huruma yake, kama alivyowaambia baba zetu, Abrahamu na uzao wake hata milele." Maria alikaa Naya [Elizabeti] kadiri ya miezi mitatu, Kisha akarudi nyumbani kwake.
Injili ya Bwana.