SOMO 1
Isaya 7:10—14
Siku zile: Bwana alimwambia Ahazi maneno haya: Ujiombee ishara kwa Bwana Mungu wako; "Sitaomba! Wala sitamjaribu Bwana!" Hapo Bwana akamwambia: Sikilizeni sasa, enyi nyumba ya Daudi! Haiwatoshi kuwachokoza watu! Hata mtake kumjaribu Mungu wangu pia? Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ninyi ishara; tazameni, bikira atachukua mimba, atamzaa mwana, jina lake atamwita Emanueli.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 24:1—2, 3—4ab, 5—6
K. Bwana anaingia, yeye ndiye mfalme wa utukufu.
Nchi ni yake Bwana na vyote vinavyoijaza,
dunia yote na wakaaji waliomo.
Maana Mungu ameweka misingi yake juu ya bahari,
ameisimika juu ya mito ya maji. K.
Ni nani atakayeupanda mlima wa Bwana?
Ni nani atakayesimama mahali pake patakatifu?
Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe,
asiyeuinua moyo wake kwa mambo ya miungu. K.
Huyo atapata baraka kwa Bwana,
na tuzo ya Mungu Mwokozi wake.
Hiki ni kizazi cha wenye kumtafuta,
cha wenye kuutafuta uso wako, ee Mungu wa Yakobo. K.
SHANGILIO LA INJILI
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Ewe Ufunguo wa Daudi! Unafungua malango ya Ufalme wa milele: njoo, utuongoze kutoka katika kifungo chetu, sisi tunaoishi gizani.
W. Aleluya.
INJILI
Luka 1:26—38
Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu aende katika mji wa Galilaya uitwao Nazareti, kwa mwanamwali bikira, mchumba wa mtu, jina lake Yosefu, wa nyumba ya Daudi, na jina la huyo bikira lilikuwa Maria. Na malaika akaingia kwake, akasema, "Salamu, uliyejaa jaa neema! Bwana yu nawe." Naye akashtuka kwa sababu ya maneno hayo, na akawaza maana ya maamkio hayo. Malaika akamwambia, "Usiogope, Maria, kwa maana umebarikiwa na Mungu. Tazama, utachukua mimba na kumzaa mwana, na utampa jina Yesu. Huyo atakuwa mkubwa na kuitwa Mwana wa Aliye Juu na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi baba yake, ataitawala nyumba ya Yakobo hata milele, na utawala wake hautakuwa na mwisho." Maria akamwambia malaika, "Litakuwaje neno hili maana sijui mume?" Malaika akamjibu akisema, "Roho Mtakatifu atakushukia, na nguvu ya yule Aliye Juu itakufunika kwa kivuli chake. Kwa hiyo kitakatifu kitakachozaliwa kitaitwa Mwana wa Mungu. Hata jamaa yako Elizabeti amepata mimba ya mtoto mwanaume katika uzee wake; na huu ni mwezi wake sita kwa yeye aliyeitwa tasa; kwa maana hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu." Maria akasema, "Tazama, mimi ni mtumishi wa Bwana, nitendewe ulivyonena." Kisha malaika akamwacha, akaenda zake.
Injili ya Bwana.