SOMO 1
Waamuzi 13:2—7, 24—25a
Siku zile, palikuwa na mtu mmoja wa Zora, wa kabila la Dani jina lake Manoa, na mkewe alikuwa tasa, wala hakuzaa mtoto. Malaika wa Bwana akamtokea huyo mwanamke akamwambia, "Tazama wewe umekuwa tasa, wala hukuzaa, lakini sasa utachukua mimba na utamzaa mtoto kiume. Basi sasa jihadhari nakusihi, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi; kwa maana tazama, utachukua mimba, utamzaa mtoto mwanaume, na wembe usipite juu ya kichwa chake, kwa sababu mtoto huyo atakuwa mnadhiri wa Mungu tangu tumboni mwa mama yake, naye ataanza kuwaokoa Waisraeli kutoka katika mikono ya Wafilisti." Ndipo huyo mwanamke akaenda na kumwambia mume wake, "Mtu wa Mungu alinijia, sura yake ilikuwa kama ya malaika yenye kuogopesha. Mimi sikumuuliza ametoka wapi, wala hakuniambia jina lake. Lakini akaniambia, 'Tazama, utachukua mimba na kumzaa mtoto mwanaume; hivyo tangu leo usinywe tena divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi. Kwa maana mtoto huyo atakuwa mnadhiri wa Mungu tangu tumboni mwa mama yake, hadi siku ya kufa kwake.'" Ikawa mwanamke huyo akamzaa mtoto wa kiume, akamwita jina lake Samsoni; naye alipokua, Bwana akambariki. Roho ya Bwana ikaanza kumjia.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 71:3—4a, 5—6ab, 16—17
K. Kinywa changu kitajazwa sifa zako na utukufu wako.
Uwe kwangu mwamba wa kukimbilia,
nitakakokwenda siku zote; umeamuru niokolee,
maana wewe ni mwamba wangu na ngome yangu.
Ee Mungu wangu, uniopoe mkononi mwa mwovu. K.
Kwani ee Mwenyezi Bwana, ndiye tumaini langu;
nimekuaminia, ee Bwana, tangu ujana wangu.
Nimekutegemea wewe tangu kuzaliwa;
ndiwe nguvu zangu tangu tumboni mwa mama yangu. K.
Nitakuja na kutangaza matendo makuu ya Bwana;
ee Mwenyezi Bwana, nitahubiri haki yako wewe peke yako.
Ee Mungu, umenifundisha tangu ujana wangu;
mpaka sasa nimeyatangaza maajabu yako. K.
SHANGILIO LA INJILI
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Ewe Chipukizi la Yese, unayesimama kama ishara ya mataifa, njoo na utuokoe, usikawie zaidi.
W. Aleluya.
INJILI
Luka 1:5—25
Siku za Herode, mfalme wa Yudea, kulikuwako kuhani, jina lake Zakaria, wa zamu ya Abiya; mkewe, jina lake Elizabeti, alikuwa wa ukoo wa Haruni. Wote wawili walikuwa wacha Mungu; katika maisha yao walishika amri zote za Bwana na sheria zake bila hitilafu. Lakini walikuwa hawana mtoto, kwa maana Elizabeti alikuwa tasa na wote wawili walikuwa wazee. Ikaja zamu ya kuhudumu mbele ya Mungu, hapo, kwa desturi ya ukuhani ilipigwa kura, nayo ilimwangukia yeye aingie katika hekalu la Bwana na kufukiza ubani. Saa ya kufukiza ubani, umati wa watu walikuwa wakisali nje. Mara malaika wa Bwana akamtokea upande wa kulia wa altare ya kufukizia. Zakaria alipomwona, alifadhaika, akashikwa na hofu. Lakini malaika akamwambia, "Usiogope, Zakaria, sala yako imesikilizwa. Elizabeti, mke wako, atakuzalia mwana, naye umwite Yohane. Nawe utafurahi na kushangilia, na wengi watafurahia kuzaliwa kwake, kwa maana atakuwa mkubwa mbele ya Bwana. Hatakunywa divai wala kileo. Atajazwa Roho Mtakatifu tangu tumboni mwa mama yake, na wengi wa wana wa Israeli atawarejeza kwa Bwana, Mungu wao. Atamtangulia Bwana katika roho na nguvu ya Eliya, ili kuelekeza mioyo ya akina baba kwa wana wao, na waasi kujali haki, na kumtayarishia Bwana watu walioandaliwa." Zakaria akamwambia malaika, "Namna gani nitahakikisha hayo." Maana mimi ni mzee, na mke wangu amepita siku zake." Malaika akamjibu akisema, "Mimi ni Gabrieli nisimamaye mbele ya Mungu. Nimetumwa niseme nawe na kukupasha habari hii ya furaha. Tazama, kwa sababu husadiki maneno yangu yatakayotimia wakati wake, utakuwa bubu, wala hutaweza kusema mpaka siku yatakapotendeka hayo." Muda huo wote watu walimsubiri Zakaria nje na wakashangaa kwa sababu alikawia mno hekaluni. Alipotoka, hakuweza kusema nao, basi wakang'amua ya kuwa ameona maono hekaluni. Naye akawaashiria, akaendelea kuwa bubu. Siku zake za huduma zilipomalizika, alirudi nyumbani kwake. Baada ya siku zile, mkewe Elizabeti alichukua mimba, akakaa ndani ya nyumba miezi mitano, akisema, "Hivyo ndivyo Bwana amenitendea siku alipoona imefaa kuondoa aibu yangu mbele ya watu."
Injili ya Bwana.