SOMO 1
Yeremia 23:5—8
Tazama, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapomwoteshea Daudi chipukizi takatifu, mfalme atakayetawala na kutenda kwa hekima, na kufanya hukumu na haki katika nchi. Siku zake, Yuda ataokolewa, na Israeli atakaa salama, naye ataitwa jina hili: "Bwana ndiye haki yetu." Basi angalieni, siku zinakuja — asema Bwana ambapo hawatasema tena, "Kama Bwana anavyoishi, aliyewahamisha wana wa Israeli kutoka nchi ya Misri." Lakini watasema, "Kama Bwana anavyoishi, aliyewahamisha na kuwarudisha wazao wa nyumba ya Israeli, kutoka nchi ya kaskazini — na kutoka nchi zote, alikowafukuzia kwanza," ili wakae tena katika nchi yao wenyewe.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 72:1—2, 12—13, 18—19 (K. tazama 7)
K. Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi na wingi wa amani milele.
Ee Mungu, umpe mfalme hukumu yako,
na mwana wa mfalme haki yako;
ahukumu taifa lako kwa haki,
na wanyonge kwa usawa. K.
Maana atamkomboa maskini mwenye kumlilia,
na mnyonge asiye na msaidizi.
Atamhurumia dhaifu na mhitaji,
ataziokoa nafsi za wahitaji. K.
Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli,
yeye peke yake afanyaye maajabu.
Jina lake tukufu lihimidiwe milele,
dunia nzima ijae sifa yake. K.
SHANGILIO LA INJILI
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Ewe Kiongozi wa nyumba ya Israeli, uliyempa Musa amri zako juu ya mlima Sinai, uje kutuokoa kwa mkono wako wenye nguvu.
W. Aleluya.
INJILI
Mathayo 1:18—24
Kuzaliwa kwa Yesu Kristo kulikuwa hivi. Maria, mama yake, alipokuwa ameposwa na Yosefu, kabla hawajakaa pamoja alionekana ana mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Mumewe Yosefu akiwa mtu mwadilifu, hakupenda kumwaibisha hadharani. Basi, akanuia kumwacha kwa Siri. Alipokuwa akifikiria hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea ghafla katika ndoto, akasema, "Yosefu, mwana wa Daudi, usiogope kumpokea Maria kuwa mke wako, maana mimba yake ameipata kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Atamzaa mwana, nawe utampa jina lake "Yesu." Maana yeye atawaokoa watu wake katika dhambi zao." Hayo yote yametendeka, ili neno alilonena Bwana kwa njia ya nabii litimie, kwamba "Tazama, bikira atachukua mimba na kumzaa mwana, naye watamwita Emanueli," maana yake, "Mungu pamoja nasi." Yosefu alipoamka kutoka usingizini, alifanya kama malaika wa Bwana alivyomwagiza.
Injili ya Bwana.