SOMO 1
Isaya 61:1—2a, 6a, 10—11
Roho wa Bwana Mungu yu juu yangu, kwa sababu Bwana amenipaka mafuta. Amenituma niwahubirie maskini habari njema, kuwaponya waliovunjika moyo: kuwatangazia mateka uhuru, na wafungwa kuwa huru, kutangaza mwaka wa rehema ya Bwana. Nitafurahi sana katika Bwana, roho yangu itamshangilia Mungu wangu. Maana amenivika mavazi ya wokovu, amenifunika vazi la utakatifu, kama bwana harusi anavyojipamba taji, na kama bibi harusi anavyojivika mapambo yake. Kama vile udongo unavyotoa machipuko yake, na kama vile bustani inavyootesha mbegu zake, hivyo Bwana Mungu ataotesha utakatifu, na sifa mbele ya mataifa yote.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
LUKA 1:46—48, 49—50, 50, 53—54
K. Roho yangu itamshangilia Mungu wangu.
Au: Mwenye heri Bikira Maria, uliyemchukua Mwana wa Baba wa milele!
Moyo wangu wamtukuza Bwana;
na roho yangu imeshangilia katika Mungu, Mkombozi wangu.
Kwa kuwa ameangalia unyonge wa mtumishi wake;
tazama, toka sasa vizazi vyote wataniita mwenye heri. K.
Kwa maana amenitendea makubwa Aliye Mwenyezi,
na jina lake ni takatifu.
Na huruma yake ipo toka kizazi hata kizazi
kwa wale wenye kumcha. K.
Wenye njaa amewashibisha mema,
matajiri amewarudisha mikono mitupu.
Amemsaidia Israeli, mtumishi wake,
akiikumbuka huruma yake. K.
SOMO 2
1 Wathesalonike 5:16—24
Ndugu zangu: Furahini kila wakati. Salini bila kuchoka. Fanyeni shukrani katika vyote: hayo ndiyo atakayo Mungu kwenu katika Kristo Yesu. Msimzime Roho. Msiidharau karama ya unabii. Kagueni yote: yaliyo mema yashikilieni. Mabaya ya kila namna yaepukeni. Naye Mungu wa amani awatakase na kuwakamilisha, mpate kuhifadhiwa salama roho, moyo na mwili bila hitilafu mpaka kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye aliyetuita ni mwaminifu, atatimiza neno lake.
Neno la Bwana.
SHANGILIO LA INJILI
ISAYA 61:1
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Roho wa Bwana yu juu yangu, amenituma niwahubirie maskini habari njema.
W. Aleluya.
INJILI
Yohane 1:6—8, 19—28
Palitokea mtu, ametumwa na Mungu, jina lake Yohane. Huyo alikuja kutoa ushuhuda, apate kuushuhudia mwanga ili wote wasadiki kwa sababu yake. Yeye hakuwa ule mwanga. Huu ndio ushuhuda wa Yohane. Wayahudi walipowatuma makuhani na Walawi kutoka Yerusalemu waende kwake na kumwuliza, "Wewe u nani?" Naye alikiri, wala hakukana; basi akakiri akajibu, "Mimi si Kristo." Wakamwuliza, "Wewe u nani basi? Wewe u Eliya?" Akasema, "Hapana," "Wewe u nabii yule?" Akajibu, "La!" Basi, wakamwambia, "U nani wewe? Tupate kuwapa majibu wale waliotutuma. Wewe mwenyewe wajisema kuwa nani?" Akasema, "Mimi, ni kama alivyonena nabii Isaya — 'ndiyo sauti ya mtu aliaye nyikani, inyosheni njia ya Bwana.'" Nao wajumbe walikuwa wa jamii ya Mafarisayo. Wakaendelea kumhoji na kumwambia, "Mbona basi, wabatiza, ikiwa wewe si Kristo, wala Eliya, wala nabii yule?" Yohane akawajibu, "Mimi nabatiza kwa maji. Katikati yenu amesimama yeye msiyemjua ninyi, yeye ndiye anayekuja nyuma yangu, ambaye sistahili kufungua ukanda wa kiatu chake." Mambo hayo yalitendeka Bethania, ng'ambo ya Yordani, alikobatiza Yohane.
Injili ya Bwana