SOMO 1
Isaya 48:17—19
Bwana aliye Mkombozi wako, Mtakatifu wa Israeli asema: Ndimi Bwana, Mungu wako, ninayekufundisha ili upate ufanisi, ninayekuongoza katika njia inayofaa. Ungalisikiliza maagizo yangu, amani, yako ingalikuwa kama mto wa maji, na haki yako kama mawimbi ya bahari. Wazao wako wangalikuwa kama mchanga, nao waliozaliwa nawe kama chembe, jina lako halitafutwa hata, wala halitafutwa mbele yangu.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 1:1—2, 3, 4 na 6
K. Akufuataye, ee Bwana, atakuwa na nuru ya uzima.
Heri mtu yule
asiyefuata shauri la waovu,
asiyesimama katika njia ya wakosefu,
wala kukaa katika baraza la wenye mzaha.
Bali, furaha yake ni katika sheria ya Bwana,
na kuitafakari sheria yake mchana na usiku. K.
Naye ni kama mti uliopandwa
kandokando ya vijito vya maji,
unaozaa matunda kwa wakati wake,
wala Jani lake halinyauki;
kila wafanyalo linafanikiwa. K.
Sivyo walivyo waovu!
Wao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.
Maana Bwana anatunza njia yao waadilifu,
lakini njia ya waovu iyapotea. K.
SHANGILIO LA INJILI
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Bwana anakuja, mkimbilie ukamlaki;
yeye ni Mfalme wa amani.
W. Aleluya.
INJILI
Mathayo 11:16—19
Wakati ule: Yesu aliuambia umati wa watu: "Nifananishe kizazi hiki na nini? Kimefanana na watoto wakaao sokoni na kuwaita wenzao, wakisema, 'Tuliwapigia filimbi, nanyi hamkucheza; tuliomboleza, nanyi hamkulia.' Maana Yohane alikuja, hakula wala hakunywa, nao wakasema, 'Ana Pepo mbaya.' Mwana wa Mtu amekuja anakula na kunywa, nao wanasema, 'Mlafi huyu na mlevi, rafiki yao watoza ushuru na wakosefu.' Hekima inathibitishwa kuwa ina haki kwa matendo yake."
Injili ya Bwana.