SOMO 1
Isaya 41:13—20
Mimi Bwana, ndimi Mungu wako, ninayeshika mkono wako wa kulia; ninayekuambia: Usiogope, nitakusaidia. Usiogope, ewe mdudu wa Yakobo, ewe funza Israeli: kwani mimi nitakusaidia, asema Bwana; Mkombozi wako ni Mtakatifu wa Israeli. Tazama, nimekufanya kuwa gari la kupendea, gari jipya lenye meno makali kuwili, utaponda milima na kuisaga, utafanya vilima kuwa kama makapi. Utavipepeta, upepo utavipeperusha, tufani itavisambaza. Nawe utamfurahia Bwana; utajitukuza katika Mtakatifu wa Israeli. Wanyonge na maskini wanatafuta maji, wala hakuna, ndimi zao zimekauka kwa kiu. Mimi, Bwana, nitawajibu, mimi, Mungu wa Israeli, sitawaacha. Katika mahali pakavu nitatiririsha mito, na chemichemi za maji katikati ya mabonde. Nitageuza jangwa kuwa ziwa la maji, na nchi kavu kuwa visima. Katika jangwa nitatia mwerezi, mkakaya, mkingu na mzeituni; katika nyika nitaweka pamoja mvinje na mparamusi na misonobari. Ili watu waone na kujua, ili waangalie na kutambua, ya kuwa mkono wa Bwana umefanya hayo, Mtakatifu wa Israeli ameyaumba.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 145:1 na 9, 10—11, 12—13ab
K. Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma na rehema.
Nitakutukuza, ee Mungu wangu mfalme;
nitalisifu jina lako daima na milele.
Bwana ni mwema kwa wote,
na huruma yake i juu ya viumbe vyake vyote. K.
Kazi zako zote zinakutukuza, ee Bwana,
wachaji wako wanakusifu.
Wanautaja utukufu wa ufalme wako,
wanauhadithia uwezo wako. K.
Ili wawajulishe wanadamu matendo yako makuu,
na fahari tukufu ya ufalme wako.
Ufalme wako ni ufalme wa nyakati zote,
na utawala wako wadumu kwa vizazi vyote. K.
SHANGILIO LA INJILI
TAZAMA ISAYA 45:8
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Enyi mbingu, dondosheni chini ushindi mfano wa umande, na mawingu yaunyeshe huo ushindi kama mvua. Nchi ifunguke, upate kuleta Mkombozi.
W. Aleluya.
INJILI
Mathayo 11:11—15
Wakati ule, Yesu aliuambia umati: "Amin, nawaambieni, katika wote waliozaliwa na mwanamke hajapata kutokea mtu aliye mkubwa kuliko Yohane Mbatizaji. Lakini katika ufalme wa mbingu, mdogo wa mwisho ni mkubwa kuliko yeye. Tangu siku za Yohane Mbatizaji hata sasa, ufalme wa mbingu hupatikana kwa juhudi tu, nao wenye juhudi ndio wanaounyakua. Kwa maana manabii wote na sheria walitabiri mpaka wakati wa Yohane
Naye — mkitaka kuniamini — ni Eliya atakayekuja. Aliye na masikio, na asikie."
Injili ya Bwana.