KUMBUKUMBU YA MT. ALFONSI WA LIGUORI, ASKOFU NA MWALIMU WA KANISA, AGOSTI 1, 2024
LITURGICAL COLOUR: WHITE 🤍
SOMO LAKWANZA
YEREMIA 18:1—6
Kama vile udongo ulivyo katika mkono wa mfinyanzi, ndivyo mlivyo katika mkono wangu.
Somo katika kitabu cha Nabii Yeremia
Neno hili lilimfikia Yeremia kutoka kwa Bwana, likisema: Simama, ukateremke mpaka nyumba ya mfinyanzi, na huko nitakupasha maneno yangu." Basi nikateremka mpaka nyumba ya mfinyanzi, na tazama, alikuwa akifanya kazi kwa magurudumu mawili. Lakini chungu alichokuwa anakifinyanga kiliharibika, naye akaanza mara ya pili, na kwa udongo uliokuwa katika mikono yake akafanya chungu kingine, kama alivyoona vema kukifanya. Hapo neno la Bwäna likanifikia, likisema: "Ewe nyumba ya Israeli, je, mimi siwezi kuwatendea ninyi sawasawa na mfinyanzi huyu? - asema Bwana. Tazama, kama vile udongo ulivyo katika mkono wa mfinyanzi, ndivyo mlivyo katika mkono wangu, ewe nyumba ya Israeli."
NENO LA BWANA... TUMSHUKURU MUNGU
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 146:2, 34, 5—6 (K. 5a)
K. Heri ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake.
Umsifu Bwana, ee nafsi yangu;
nitamsifu Bwana maisha yangu yote,
nitamwimbia Mungu wangu zaburi muda ninaoishi. K.
Msiwatumainie wakuu,
wala mwanadamu asiyeweza kuokoa.
Pumzi yake inapotoka, huurudia udongo wake,
siku hiyo mashauri yake yanapotea. K.
Heri ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake,
ambaye tumaini lake ni kwa Bwana, Mungu wake,
yeye alizifanya mbingu na nchi,
bahari na vyote vilivyomo. K.
SHANGILIO LA INJILI
TAZAMA MATENDO YA MITUME l6:14b
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Fungua mioyo yetu, ee Bwana, tupate kuyasikiliza na kuyapokea mafundisho ya Mwanao.
W. Aleluya.
SOMO LA INJILI
MATHAYO 13:47—53
Waliwakusanya samaki wazuri katika vyombo, bali wabovu waliwatupa.
† Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Mathayo
Wakati ule: Yesu aliwaambia makutano, "Ufalme wa mbingu umefanana na wavu uliotupwa baharini, ukanasa wa kila aina. Ulipojaa, [wavuvi] waliuvuta pwani, wakaketi, wakawakusanya samaki wazuri katika vyombo, bali wabovu waliwatupa. Ndivyo itakavyokuwa mwisho wa dunia. Malaika watakwenda kuwatenga waovu na waadilifu. Wakiwatupa waovu katika tanuri ya moto. Humo mtakuwamo kulia na kusaga meno. Mmeelewa hayo yote?" Wakamwambia, "Ndiyo, tumeelewa." Akajibu, "Kwa hiyo, kila mwandishi apataye kuwa mfuasi wa ufalme wa mbingu anafanana na mkuu wa familia atoaye mapya na ya kale katika hazina yake." Baada ya kumaliza mifano hiyo, Yesu alitoka huko.
INJILI YA BWANA... SIFA KWAKO EE KRISTO