RANGI YA KILITURJIA: ZAMBARAU
SOMO LA KWANZA
2 WAFALME 5:1—15
Palikuwa na wakoma wengi katika Israeli wakati wa nabii Elisha, lakini hakutakaswa hata mmoja wao, ila Naamani, mtu wa Shamu.
Somo katika kitabu cha pili cha Wafalme
Siku zile: Naamani, jemadari wa jeshi la mfalme wa Aramu alikuwa mtu mkubwa mbele ya bwana wake, na mwenye kuheshimiwa, kwa maana kwa mkono wake Bwana aliwapatia Waaramu ushindi dhidi ya adui zao. Lakini pamoja na uhodari wake wa vita alikuwa na ukoma. Ikawa Waaramu wakatuma vikosi kushambulia nchi ya Israeli, nao wakamchukua mateka msichana mdogo wa Israeli, amabye alimhudumia mke wa Naamani. Akamwambia bi mkubwa wake, “Laiti bwana wangu angeonana na nabii yule anayekaa Samaria! Angemponya ukoma wake.” Naamani akamwarifu bwana wake akisema, “Yule kijana mwanamke aliyetoka nchi ya Israeli asema hivi na hivi.” Mfalme wa Aramu akamwambia, “Nenda! Nami nitaandika barua utakayoichukua kwa mfalme wa Israeli.” Basi Naamani akaenda zake, akachukua pamoja talanta kumi za fedha na vipande vya dhahabu elfu sita na mavazi kumi ya nguo. Akampa mfalme wa Israeli ile barua iliyosema, “Barua hii itakapokufikia utambue kuwa nimetuma kwako mtumishi wangu Naamani ili uweze kumponya ukoma wake.” Alipoisoma ile barua, mfalme wa Israeli aliyararaua mavazi yake akisema, “Je, mimi ni Mungu, mwenye kuua na kuhuisha hata mtu huyu anipelekee mtu nimponye ukoma wake? Fahamuni basi! Nawasihi, kuwa mtu huyu anatafuta ugomvi nami!” Mtu wa Mungu Elisha, aliposikia kuwa mfalme wa Israeli amerarua mavazi yake, akamtumania ujumbe mfalme, “Kwanini umerarua mavazi yako? Umtume kwangu, ili apate kujua kuwa katika Israeli kuna nabii.” Naamani akafika na farasi wake na magari yake, akasimama mlangoni pa Elisha. Elisha akamtumia ujumbe akisema, “Nenda ukaoge katika Yordani mara saba, na nayama ya mwili wako itarudi kama zamani, nawe utakuwa umetakata.”lakini Naamani akakasirika, akaondoka zake, akisema, “Tazama, nilidhani kuwa, hakika atatoka nje na atakuja mbele yangu, kasha ataomba kwa jina la Bwana Mungu wake, atasugua mahali palipo na ugonjwa kwa mkono wake, na hivyo kuniponya na ukoma. Je, maji ya Abana na Farpari, mito ya Damasko sio bora kuliko maji yote ya Israeli? Je, kama ningeoga ndani yake, si ningekuwa safi?” akageuka, akenda zake kwa hasira. Watumishi wake wakamkaribia, wakamwambia, “Babangu kama Yule nabii angalikuagiza jambo kubwa si ungalitenda? Je, si zaidi sana basi, anapokuambia, ‘uoge ukatakate’?” Basi Naamani, akashuka, akajizamisha katika Yordani mara saba kadiri ya neno la mtu wa Mungu. Mara nyama ya mwili wake ikarudi kuwa kama nyama ya mwili wa mtoto mdogo, akatakata. Hapo akamrudia Yule mtu wa Mungu, yeye na msafara wake wote. Alipofika akasimama mbele yake na kusema “Sasa nimetambua kuwa hakuna Mungu dunia kote, ila katika Isareli.”
NENO LA BWANA… TUMSHUKURU MUNGU
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 42:2, 3, 43:3, 4 (K. 42:3)
K. Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu, Mungu aliye hai; lini nitaingia niuone uso wa Mungu?
Kama ayala atamanivyo mito ya maji,
ndivyo nafsi yangu inavyokuonea kiu, wewe, ee Mungu. K.
Roho yangu inamwonea kiu Mungu,
inamwonea kiu Mungu aliye hai.
Lini nitakuja kuuona uso wake Mungu? K.
Ulete mwanga na uaminifu wako, / navyo vitaniongoza,
vitanipeleka kwenye mlima wako mtakatifu,
na kwenye makao yako. K.
Nitakwenda altareni kwa Mungu,
kwa Mungu, aliye furaha na shangwe yangu.
Nitakusifu kwa kukupigia kinubi,
Ee Mungu, Mungu wangu! K.
SHANGILIO LA INJILI
TAZAMA ZABURI 130:5, 7
W. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo.
K. Ninamngoja Bwana, na ninalitumainia neno lake, kwa maana kwa Bwana kuna fadhili, kwake kuna wokovu mwingi.
W. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo.696*
INJILI
LUKA 4:24—30
Kama Eliya na Elisha, Yesu hakutumwa kwa Wayahudi peke yao.
Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Luka.
Wakati Yesu alipokuja Nazareti, aliwaambia watu waliokuwamo katika sinagogi, “Amin, nawaambieni, hakuna nabii mwenye kukubaliwa mjini mwake. Tena, ni kweli ninavyowqaambia, palikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli zamani za nabii Eliya, wakati mbingu zilifungwa miaka mitatu na miezi sita hata njaa kali ikaingia nchi nzima. Lakini Eliya hakutumwa kwa mmojawapo, ila kwa mwanamke mjane wa Zarefathi katika nchi ya Sidoni. Kadhalika, walipatikana wakoma wengi katika Israeli wakati wa nabii Elisha, lakini hakutakaswa hata mmoja wao, ila Naamani, mtu wa Shamu.” Hapo wote wenye kusikia hayo katika sinagogi walishikwa na hasira. Wakasimama, wakamchukua mpaka nje ya mji kwenye ukingo wa kilima, ambacho mji umejengwa, ili wamtupe chini. Yeye lakini, alipita katikati yao, akaneda zake.
INJILI YA BWANA… SIFA KWAKO EE KRISTO