Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika Zaburi ya wimbo wa katikati, Mzaburi anashangilia kwa sababu Mungu amekuwa mkarimu kuwaonesha mataifa wokovu wake. Tayari kwa hakika Mwenyezi Mungu amekwishaonesha ukarimu wa kuutangaza ukuu wake machoni pa mataifa yote.
Paulo katika somo la kwanza anatambua upendo huu mkuu wa Mungu wa kutaka wokovu wake utangazwe machoni pa mataifa yote na hivyo anakuwa tayari kushirikiana na Mwenyezi Mungu katika kuifanya nia hii itimie. Anajitahidi kuitangaza injili ya Bwana kila mahali. Paulo anafanya hivi kwa kutambua kwamba wanadamu wote wanatamani kupata kitu chema; wanadamu wote ni mali ya Mungu na hivyo hawapaswi kulishwa mafundisho mabaya, au kuachwa katika genge na shimo la shetani. Nasi tujione kama Paulo kwamba wokovu umekwishatangazwa kwa wote. Hivyo watu wote wanapaswa kulishwa kitu chema na sio makapi.
Hata kama ni chakula wanapaswa kulishwa chakula chema, kama ni maji, au elimu wanahitaji kupewa vitu bora. Na sio mauchafu. Hivyo tujifunze kutoa kwa wenzetu vitu vyema. Mtu asipewe uchafu kwa sababu ati ni maskini, wanadamu wanapaswa kulishwa kitu chema.
Katika injili, Yesu anamsifu kadhi aliyetumia cheo chake kujenga urafiki na wenzake ili basi apate wa kumkaribisha endapo mambo yanakuwa magumu. Hakika huyu alitumia ujanja wake, vipaji vyake vya kuzaliwa na cheo chake kujijengea urafiki na wenzake. Nasi tutumie vipaji vyetu, elimu yetu na afya yetu katika kujenga urafiki na Mungu. Vipaji vyetu na elimu yetu ni hazina kubwa. Tukivitumia vyema twaweza kumkaribia Mungu kwa karibu zaidi na kubarikiwa naye.
Wengi wetu tunavitumia vipaji vyetu kujiweka mbali zaidi na Mwenyezi Mungu. Tunatumia fedha zetu kwa ajili ya uasherati na vipaji vyetu kujivuna zaidi na hivyo kuharibu mahusiano yetu na wenzetu na kuharibu afya zetu. Pale tupewapo fedha baadhi tunazitumia kwa kwa dhambi. Yafaa tubadilike. Tutumie vyote kwa ajili ya Bwana.
©️ Pd. Prosper Kessy OFMCap.