Iko hivi...
Wengi tumekuwa tukishangaa mavazi ya Mapadre, vitambaa na vitu mbalimbali vya Ibada kuwa na alama hiyo, kama ilivyo kwenye hiyo picha hapo chini. Leo nataka nikujuze kidogo maana yake na historia yake, hivyo nakusihi ujitahidi usome mpaka mwisho. Maneno yasiwe mengi. "IHS" ni ufupisho wa Jina Takatifu la Yesu kwa Kigiriki "IΗΣΟΥΣ" na imeanza kutumika tangu karne ya pili mpaka leo karne ya 21.
Kwani kabla kipindi cha Wakristo kuteswa na kuuawa na utawala wa kidhalimu wa Kirumi, maandishi hayo yalitumiwa kama alama ya siri (secret code) katika nyumba, makaburi na Makanisa ya siri ya Wakristo. Nao Wakristo wakiiona, iliwarahisishia kujua kuwa hapo ndio kwao.
Mtakatifu Bernadine wa Siena (1380-1444) na Mwanafunzi wake Mtakatifu Yohane wa Capistrano (1386-1456) walitumia alama hiyo kueneza Ibada ya Jina Takatifu la Yesu. Miujiza mingi sana ilitendeka kupitia alama hiyo, hadi kuwafanya watu wengine kuhisi kuwa ni ushirikina. Ndipo mnamo mwaka 1427, Papa Martin V alipopitisha Ibada hii na akaelekeza iwekwe pia na Msalaba katikati yake, kama ilivyo kwenye hiyo picha hapo chini.
Watu wakashangaa inawezekanaje Jina kuponya? Yesu mwenyewe aliahidi hili: "Kwa Jina langu watatoa pepo, na kusema kwa lugha mpya. Wakishika nyoka au wakinywa kitu chochote chenye sumu, hakitawadhuru. Watawekea wagonjwa mikono, nao watapona" (Marko 16:17-18).
Pia ukipata muda, soma Mdo 2:21, Mt 4:1-11, Yoh 16:23-24 na Kol 3:17.
Lakini kutokana na kufifia kwa lugha ya Kigiriki duniani, na lugha ya Kilatini kushamiri, ndipo alama hiyo ya "IHS" ikatafsiriwa kama "Iesus Hominum Salvator" yaani "Yesu Mwokozi wa wanadamu" bila kupoteza maana yake ile ile ya mwanzo. Kumbuka alama hiyo ipo kwa ajili ya kutangaza tu Ukuu wa Jina Takatifu la Yesu, na sio vingenevyo.
...TUMSIFU YESU KRISTO...