Familia Takatifu
Leo ni Dominika ya kuangalia maisha ya ndani ya familia ya Nazarethi aliyoishi Yesu. Tunu za familia hii zinapaswa ziigwe na familia zetu. Duniani wengi tunataka familia zetu zifanane na za watu maarufu na hivyo tunajikuta tukiiga hata mabaya ya familia hizi. Leo, Kanisa linatualika tuige maisha ya Yesu, Maria na Yosefu. Tunayo matatizo mengi ndani ya familia kwa sababu ya kuiga mifano mibaya. Sherehe ya mwaka huu umepanga ikubadilishe vipi? Sisi tunaoadhimisha sherehe hii kila mwaka, je, tumebadilika?
Familia Takatifu ikusute uone kwamba kweli wewe unahitaji mabadiliko maishani mwako. Kwenye familia usimchukulie yeyote kimzaha-kila mmoja apatiwe heshima yake na hata yule anayejionesha kana kwamba hapendi heshima sana, asiache kupatiwa heshima yake. Hakuna binadamu asiyependa kuheshimiwa. Wote wanataka watambulike na kuheshimiwa. Pili, lazima mioyo yetu itangaze msamaha kwa sababu wanafamilia sio malaika. Hivyo, tuwe tayari kusameheana. Shetani akitaka kukuumiza, siku zote atatafuta yule mtu unayemwamini sana ili akufanyie jambo la kukukwaza upate kuumia. Hivyo ujiandae kumpokea na kumsamehe hata kama ni mwanafamilia. Katika familia tusiache kuadhimisha matukio fulani pamoja. Lazima tuwe na sherehe na matukio ya pamoja.
Tuziombee familia zetu leo zipate kweli kuwa familia zenye nguvu ili zisivunjwe na magumu na matatizo. Matatizo na changamoto yamevunja familia zetu nyingi lakini sisi tujiombee ili matatizo ya namna hii yapate kutujenga zaidi na zaidi. Tambua kwamba kufanikiwa kulea familia ni moja ya mafanikio makubwa sana duniani. Waweza kufanikiwa kupata kazi na kuajriwa sehemu mbalimbali lakini kama utashindwa kuilea familia yako, mafanikio yako yatabakia kuwa magumu bado.
©️Pd. Prosper Kessy OFMCap.