Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo tuna adhimisha kumbukumbu ya Mt. Elizabeth wa Hungari, alizaliwa mwaka 1207, alikuwa mama wa familia, aliishi maisha ya unyoofu na ya kawaida ingawaje aliolewa katika familia ya kifalme, akijitoa kwa maisha ya sala, na maisha ya sadaka na hata baada ya mume wake kufariki aliamua kujitoa kuwahudumia maskini na wagonjwa na alijiunga na Utawa wa tatu wa Mt. Fransisko(Wasekulali), alifukuzwa nyumbani baada ya kuonekana kama vile anakosa hekima kwa kutumia mali ya mume wake kuwasaidia maskini. Alifariki mwaka 1231. Kuwasaidia maskini kunaonekana kama ukosefu wa hekima kwa Mt. Elizabeth.
Neno la Bwana katika asubuhi ya leo tukianza kwa kuliangalia somo la kwanza. Hapa tunamkuta mwandishi akiwalaumu wale ambao katika jamii yake walionekana kama wataalamu wa mambo, kama wajuzi na waliheshimika na kila mtu. Hawa waliweza kufanya utabiri wa vitu vingi, kutibu hata magonjwa makubwa, kuongea maneno ya kuvutia watu sana. Lakini cha ajabu ni kwamba walishindwa kumwona Mungu katika viumbe vyake, walishindwa kujua kwamba viumbe vinatangaza utukufu wa Mungu kama tunavyoelezwa katika zaburi ya wimbo wa katikati. Hili walishindwa ndugu zangu.
Sasa mwandishi wa kitabu hiki anashangaa kwani watu hawa bado ndio wanaonekana kwamba wana hekima, kama waheshimiwa lakini ki ukweli hakuna kitu kabisa. Hawa watu ni sifuri kabisa.
Somo la injili ni mwendelezo wa maada kama hii. Hapa tunakuta tena habari juu ya watu wanavyokosa kuwa na hekima, tena ni wale ambao katika jamii wanaonekana kama wajanja. Injili inatuambia kwamba hawa ndio wanaoongoza kwa kukosa hekima na katika kila dhoruba wanakamatwa. Kwa mfano katika ile dhoruba ya Nuhu, Nuhu alionekana kama kachanganyikiwa, kama aliyekosa kazi na hakuna aliyemsikiliza. Wale wajanja ndio walionekana kuwa watu. Lakini dhoruba imekuja, wamekamatiwa huko na kufa wote. Na siku za ujio wa pili wa Masiha Yesu anasema kwamba zitakuwa hivyo hivyo, kutakuwa na aina za watu, wale wanaojiona wajanja, wenye hekima watakamatwa kama ilivyokuwa siku za Nuhu.
Ndugu zangu, masomo yetu ya leo yanatuambia kwamba tutumie hekima zetu vizuri tukijiandaa kwa ujio wa pili. Usiridhike ukiona kwamba unaitwa bosi bosi, wewe unajua habari yote ya mjini, wewe kila sherehe unaalikwa, wewe ni maarufu, kanisani unaitwa kama kamheshimiwa halafu ufikiri kwamba umesha ipata mbingu. Tulia ndugu yangu. Fikiria maisha yako. Angalia ni nani anayekuita mjanja. Unaweza kukuta unaitwa na wezi wenzako kwamba wewe ni mjanja na kichwa kikavimba na kujisahau na kuona kwamba wewe ni kila kitu. Angalia utashangaa mwenzako anatwaliwaa na wewe waachwa.
Kingine ni juu ya toba. Kwa kweli toba inaokoa. Anayefanya toba hataachwa na Mungu hata siku moja. Tukifanya toba kwa nguvu zote, nakwambia Mungu hatatuacha kabisa, haachagi mtu yeyote. Tumesikia kwamba wako watu wawili wamelala lakini mmoja atatwaliwa. Kwa kweli anayefanya toba atatwaliwa tu. Mungu hatamwacha. Hii ni kwa sababu Mungu ni mwenye huruma nyingi mno na kila afanyaye toba atabahatika kumwona. Hivyo, tunapojiandaa kwa ujio wa pili, toba ni muhimu. Ukisoma kitabu cha Ufunuo, sura ya tatu, utatambua kwamba Yesu analiagiza kila kanisa lililo na dhambi kwamba litubu. Tutubu jamani.
Kila mtu anadhambi zake jamani. Wengine tumewaonea wenzetu kazini, tumewasengenya, tumewafanya wenzetu wachukiwe na wengine, tumewaonea wafanyakazi wetu wa ndani, tumekataa kuwatunza wazazi wetu, huku tukijitamba mjini kwamba tuna fedha na kusifiwa na watu na kuonekana wenye hekima, wakati wazazi kijijini au nyumbani wanakufa njaa. Tuache maisha hayo nakuanza ukurasa mpya leo.
©️Pd. Prosper Kessy OFMCap.