Jiandae kwa Ujio wa Siku ya Bwana
Ujumbe wa neno la Mungu tunaokutana nao leo ni juu ya kujiweka tayari kwa ujio wa Siku ya Bwana. Yesu katika injili anatuambia kwamba siku hiyo ni siku ya kutoa hesabu juu ya kile ulichokabidhiwa na Mungu, Mungu atauliza, Je, ulitumia vipi kile nilichokupa? Nipatie hesabu yako. Yesu anaonyesha katika injili kwamba hategemei sote tuzalishe kitu kinacholingana bali anataka kuona kwamba tulifanya kitu na kile alichotugawia. Kama watu tunaoisubiria siku hiyo, yabidi kubakia imara katika kumtumainia Bwana. Ndicho tunachoelezwa katika neno la Bwana kwenye Dominika yetu ya leo.
Wimbo wa mwanzo unatoka katika kitabu cha nabii Yeremia 29 “mawazo ninayowawazia ninyi ni mawazo ya Amani.” Hii ni sehemu ya ujumbe wa barua iliyoandikwa na Nabii Yeremia kwa wana wa Yuda waliokuwa wamepelekwa utumwani Babuloni. Anawaambia kwamba wakiwa huko utumwani watulie kwani bado Bwana anawawazia makubwa na hajawatupa. Wakimuita atazidi kuwaitikia; na ipo siku atakuja kuwatoa na kuwarudisha katika nchi yao.
Zaburi yetu ya wimbo wa katikati inatoa picha ya maisha ya mtu aliye na imani jinsi yanavyokuwa katika Bwana. Siku zote huwa katika mikono salama yakitegemezwa na Mungu. Zaburi hii ni fundisho kwetu kwamba nasi tunapojiandaa kwa ujio wa siku ya Bwana, tukifuata tunu za Mzaburi huyu, hakika tutabarikiwa na kufika salama kule Bwana anakotutaka tuende.
Katika somo la kwanza, mwandishi anatumia mfano wa mwanamke mwenye hekima, mwanamke anayemcha Mungu kutufundisha jinsi Mungu anavyombariki yeyote amchaye. Tumesikia habari kwamba mwanamke mwema anaaminika, anatenda mema, ni mchapakazi na ni mkarimu kwa maskini. Yeye hupendwa na kutamaniwa na kila mtu. Ndivyo Mungu anavyombariki yeyote amchaye. Tunachokigundua katika hili somo ndugu zangu juu ya sifa ya huyu mwanamke ni kwamba mwanamke Mchamungu yupo tayari kutoa hesabu ya alichofanya, kama wale waliopewa talanta katika somo la injili. Kutokana na hili, yeye huzidi kubarikiwa na kuaminiwa.
Somo la injili linakamilisha kile tulichoanza kusikia katika nyimbo na masomo yetu ya leo hasa katika somo la kwanza. Yesu anatoa mfano wa watumwa waliopewa talanta wazifanyie kazi. Wawili walizifanyia kazi na mmoja hakuzifanyia kazi. Mwishowe tunaona kwamba wale walioonesha uwajibikaji-walibarikiwa zaidi, waliendelea kuzidishiwa na kuaminiwa zaidi bali yule asiyezifanyia kazi alinyanganywa hata kile kidogo alichokuwa nacho.
Ndugu zangu, tukichunguza masomo yetu ya leo, tunajifunza yafuatayo: kwanza, maisha yetu ni kutoa hesabu ya namna tulivyotumia vile tulivyokabidhiwa kama mwanamke mwema anavyotoa hesabu na kama wale waliopewa talanta walivyotoa hesabu. Hiki ndicho kitakachotokea hata ile siku yetu ya mwisho. Vyovyote tulivyokabidhiwa tutavitolea hesabu. Kama ni padre uliyekabidhiwa waamini-utaambiwa uliwaongoza vipi? Uliwafanya wawe watakatifu zaidi? Uliwaonyesha njia sahihi ya kusali, uliwaongezea roho ya sala? Kama ni mama au baba utalizwa, je, watoto wako uliwaachia mfano gani? Majirani zako uliokuwa unaishi nao uliwaachia mfano gani? Uliwakwaza? Vijana waliokuwa unaishi nao au kukutana nao popote uliwaachia mfano gani? Uliwakwaza? Kama ni daktari utaambiwa uliwatia moyo wagonjwa wangapi? Uliwafokea? Ulichelewa kwa uzembe au kutoa dawa kimakosa? Kama ni dereva utaambiwa ulisaidia je kuepusha ajali au ulikuwa mshabikiaji ili wenzako wapate ajali? Uligonga waendesha bodaboda na baiskeli kwa uzembe?
Katika kutoa hesabu hii, kama injili inavyotueleza, hatutegemewi wote tuzalishe kitu kimoja au tutoe hesabu zinazofanana. Katika injili, tumeona kwamba mfalme alitambua uwezo wa kila mmoja na ndio maana aliwapatia talanta tofauti tofauti. Kila mmoja na cha kwake. Hivyo hata sisi katika kutoa hesabu hii, hatutegemewi kutoa hesabu inayofanana bali kila mtu atatoa hasabu kulingana na opportunities alizopewa au kukutana nazo. Mungu hategemei kwamba wewe ni mwendesha bodaboda au mama ntilie halafu ategemee kitu kile kile toka kwako kama vile anavyotegemea kwa waziri au daktari. Hata kwenye kutoa shukrani-hatutegemei tutoe vinavyolingana, kila mmoja atatoa kuendana na nafasi yake. Mungu huangalia kiasi cha majitoleo tulichotumia. Aliyepewa mengi, atadaiwa mengi pia.
Pesa waliyopewa watumwa katika mfano huu ni kubwa sana. Hii kwetu yamaanisha kwamba vipaji na tunu alivyotupa Mungu ni vikubwa mno. Ni nyingi ajabu. Na ndio maana madai yake ni makubwa. Hadai makubwa kama hakutoa makubwa. Papa Benedikto XVI anasema “Wakristo hufukia vipaji vyao mara baada ya ubatizo na kipaimara.” Tunalo jukumu la kufukua vipaji hivi.
Hivyo, hata yule mtumwa wa tatu alichopewa ni kikubwa lakini yeye alikuwa na shida kubwa. Inaonekana aliona wivu-kwa nini hawa wengine wapewe zaidi halafu mimi nipewe kidogo? Inaonekana alikuwa na historia mbaya ya malumbano kati yake na mfalme akilalamika kwamba mfalme anamchukia na mwishowe tunaona hata jibu alilomjibu mfalme na adhabu aliyopewa. Hili ni fundisho kwetu ndugu. Baadhi yetu tumezoea kuangalia vya wengine na kulalamika; tunafikiri kwamba Mungu anao ubaguzi. Hivyo tunabakia katika kulalamika. Labda ikitokea tupo kwenye chumba cha mtihani na gafla tukiona wenzetu wakiandika kwa haraka, mara moja twaweza kudhania kwamba wenzetu wameoneshwa majibu. Mwishowe tunaishai kufeli mitihani. Nawe ukiwa unaangalia kwa wengine siku zote, utashindwa kutumia vilivyo vyako na kushindwa kusonga mbele. Hivyo, tutumie muda kuangalia ndani yetu na kutambua rasilimali tulizonazo. Tuachane na kuangalia vya wengine bila kuangalia vya kwetu. Hata wale wanaohama madhehebu; ni wale wasioangalia neema zilizo ndani ya kanisa. Macho yao na masikio yao yapo pembeni. Mwanamke mwema ni yule anayejali alichonacho.
Mke mwema ndugu zangu anayehadithiwa katika somo la kwanza, ni mfano wa hawa waliopewa talanta wakarudisha faida. Mke mwema ni yule anayetumia talanta vizuri na hizi humfanya aaminike na mumewe na kupewa ulinzi wa nyumba yake yote kama wale waliozawadiwa na mfalme baada ya kuzalisha na talanta zao. Mke mbaya huficha talanta. Mke mwema ni Mchamungu na mchapakazi. Uzuri wa sura haumfanyi mtu awe mke mwema lakini uchaji wa Mungu humfanya mke mwema. Anayemcha Mungu hupendeza; Dhambi humfanya binadamu achakae. Kingine tunacho jifunza hasa kutoka kwa yule mtumwa wa tatu ni juu ya dhambi ya kutokutenda (sins of omission). Kwetu sisi wakristo hii ni ile dhambi ya kuona kitu kibaya kinatendeka na kukaa kimya (hayanihusu). Hapa ni kufukia talanta zetu na hapa tutadaiwa. Pia tujichunguze namna tunavyotumia rasilimali zetu. Tuepuke kuzitumia kwa ajili ya ulevi au uasherati. Maisha ni kutoa ripoti ya jinsi tulivyotumia vipaji na muda wetu.
Sala:
Baba Mungu, nisaidie nikuamini wewe na nikutafute wewe kila wakati katika sala bila kuchoka, Amina.
©️Pd. Prosper Kessy OFMCap.