“Wale waliokwenda katika giza la uvuli wa Mauti, mwanga umewaangazia”
Usiku wa leo ni usiku mzuri sana na tangu nikiwa mtoto niliufurahia na kuusubiria kwa hamu.
Nikiwa mtoto niliufurahia zaidi kwa sababu ya shamrashamra na wageni na jinsi mtoto Yesu alivyokuwa akibebwa kupelekwa horini. Lakini baadaye nilitambua uzuri na ukuu wa usiku huu-ni usiku ule ambapo Mungu alichukua ubinadamu ili mwanadamu apate kuwa Mungu. Ni usiku ambao kwa hakika ubinadamu wetu ulipatiwa tena heshima. Hivyo, tumkabidhi Mungu ubinadamu wetu apate kuubadilisha.
Zaburi ya wimbo wa katikati inatuambia kwamba tumwimbie Mungu wimbo mpya kwa hili tukio. Wewe umekuja kwake na wimbo mpya? Uje na upya mbele ya Mungu kwani Yesu amekuja kwetu. Tunapaswa tuoneshe mambo mapya leo. Moja ya ujumbe tunaoambiwa leo katika somo la kwanza ni kwamba wale waliokwenda katika giza la uvuli wa mauti-mwanga umewaangazia.
Zamani za nabii isaya, wafungwa sugu walifungwa kwenye gereza za kwenye mahandaki, palipo na giza tu. Watu wa namna hii ukiwaleta kwenye mwanga macho yao huteseka kwa kuwa wamezoea giza zaidi ya mwanga. Yesu ndiye mwanga. Macho yako yanateseka kukutana na kumtazama Yesu? Unateseka kufuata mafundisho yake? Ni watu gani wanaokufanya uishi katika giza maishani mwako?
Katika somo la injili, tunakutana na habari za kuzaliwa mtoto Yesu. Huyu mtoto amelazwa kinyenyekevu katika hori la kulishia wanyama. Kwanza kabisa tunapaswa kutambua kwamba kila tunapomtazama huyu mtoto, ndiye jibu kwa matatizo yetu yote. Matatizo gani? Umbea wetu, ulevi wetu na uvivu wetu. Mwambie mtoto Yesu ni nini unachotaka wewe akusaidie kujibu? Bwana Yesu leo anakuja kwa kila mmoja, na anataka kukugusa wewe kwa namna ya pekee.
Mwenyezi Mungu siku zote haachi kusogea karibu yetu. Hivyo, usiache kuutazama uso wa Bwana. Yesu aweza kukosa nyumba ya kulala ndani mwako lakini usikubali akose nafasi moyoni mwako. Kila mmoja anatamani kumtambua Yesu kwa undani zaidi. Hivyo, tusaidiane ili tuweze kukutana na Bwana Yesu.
Sala: Bwana, kipindi cha Noeli nakuomba niishi kwa Amani, Amina.
©️Pd. Prosper Kessy OFMCap.