Nabii Samweli anafundishwa namna ya kuijibu sauti ya Bwana “nena Bwana kwa kuwa mtumishi wako anasikia. Hili ni jibu alilofundishwa na kuhani Eli kumjibu Bwana. Sauti ya Bwana siku zote inapaswa ijibiwe namna hii.
Tuombe ili tuwe mfano mzuri katika kujibu sauti ya Bwana. Tuombe tupate kuwa mstari wa mbele katika kuitikia sauti hiyo ya Bwana.
“Ndipo niliposema tazama nimekuja kuyafanya mapenzi yako ee Bwana:” Haya ni maneno ya Zaburi ya 40. Yanafanania na jibu lililotolewa na nabii Isaya 6:8 (mimi hapa, nitume mimi). Nabii Isaya alitambua kwamba furaha yake ipo katika kulitenda neno la Bwana. Nasi tutambue kwamba uaminifu katika wito wetu ndio utakaotuletea furaha. Nabii Samueli anasaidiwa na Eli kuitambua sauti ya Bwana tofauti na Sauti ya binadamu wa kawaida. Hakika tunawahitaji kina Eli maishani wa kutusaidia kuitambua na kuijibu sauti ya Bwana. Samweli alivyoitwa na Bwana, alidhania kwamba anayeita ni mwanadamu wa kawaida na hakuchukulia mwito huu kwa umakini. Na ndivyo ilivyo na kwetu pia hadi leo. Wengi tunafikiria kwamba bado anayetuita ni mtu wa kawaida.
Tunafikiria kwamba pale tunapoonywa, anayetuonya ni wanadamu tu. Hatuwezi hata kuiona sauti ya Bwana katika kundi. Bwana Yesu yupo katika walipokusanyika watatu au wawili kwa jina lake (Mt. 18:20). Nyakati zetu hatuisikii sauti ya Bwana kwa sababu tumekuwa watu wa kuchagua. Tumejichagulia viongozi wa kuwasikiliza na aina ya mahubiri tunayotaka kusikiliza. Na wahubiri wengi wanangangania kupokea sifa toka kwa waamini wao. Wengi wetu tunayafurahia mahubiri pale yanapowasema wenzetu. Somo la pili linatueleza jinsi tunavyopaswa kuitunza miili yetu. Huwezi kuutupa mwili wako pembeni, useme kwamba mwili wangu siuhitaji. Kwa hakika unauhitaji mwili wako.
Katika somo la injili, Yohane Mbatizaji anamwonesha Yesu kwa wanafunzi wa kwanza kwamba yeye ni mwanakondoo. Kwa kusema hivi, Yohane alikumbushia juu ya yule kondoo aliyechinjwa kule Misri (Kut 12). Damu yake iliweza kumwokoa kila Myahudi aliyeonesha imani na unyenyekevu. Nasi tunaambiwa leo kwamba damu ya Yesu ndiyo yenye kuokoa na yeyote asiyejifunika kwa damu yake, shetani atamshambulia.
Na hadi leo, shetani anawashambulia wengi. Damu ya Yesu, Mwanakondoo asiye na dhambi au doa, inatuweka huru. Tendo alilolifanya Yohane la kumwonesha Yesu kwa wanafunzi wake linahitajika hadi leo. Yesu alionekana kuwa wa kawaida sana lakini Yohane aliweza kumtambulisha. Tunahitaji bidii ya kuendelea kumtambulisha Yesu kwa watu.
Pia tusione wivu kuwatambulisha wenzetu waliobarikiwa kwa vipaji fulani fulani. Wapo wengi walio na uwezo na maarifa mazuri lakini wamekosa nafasi. Tutakutana na Mwenyezi Mungu katika mazingira yetu ya kawaida. Uliwahi kujiuliza, je, kwa nini Mungu alipomtokea Musa, alitokea katika kichaka na sio katika mti mzuri?’ Yawezekana kwamba lengo lilikuwa ni kutufundisha kwamba Mwenyezi Mungu hana ubaguzi, na anavipenda vitu vinyenyekevu. Mungu aweza kusema na yeyote na kwake anayejinyenyekeza humpenda zaidi.’ Tutambue pia kwamba Yesu yupo katikati ya kundi lililokusanyika katika yeye. Hivyo, kuishi na wenzako vizuri ni kuishi na Yesu vizuri pia.
Sala:
Bwana, ninaomba unipe ujasiri na mwangaza katika utume wangu na unisaidie kukutumikia kiaminifu, Amina.
©️Pd. Prosper Kessy OFMCap.