Karibuni ndugu kwa adhimisho la Misa Takatifu. Leo, neno la Bwana tulianze kwa kuiangalia Injili yetu. Hapa tunakutana na suala juu ya kufunga na Yesu anasema kwamba wanafunzi wake hawawezi kufunga ikiwa wapo na Bwana arusi. Akishaondolewa, ndio watakapoanza kufunga. Bwana arusi ni Yesu mwenyewe. Wakiwa na Yesu ni kipindi cha wanachopaswa wafurahi, wajifunze neno lake, wamsikilize anachosema na kufundisha kwani kumjua Yesu na mafundisho yake ni kwa maana zaidi kuliko kufunga au kutolea dhabihu. Na wakati waliokuwa nao ili kujifunza toka kwake ni huu tu. Hakuna wakati mwingine kwani Yesu alikuwa hana muda mrefu duniani. Wangeishia kufuata tena na zile desturi za Kiyahudi za kufunga, wangechanganya mambo na labda mwishoni Yesu atakapokuwa ameondoka, wangeshindwa kukumbuka na kutofautisha kati ya cha Yesu na cha dini ya Kiyahudi. Ndio maana Yesu anaendelea kusema kwamba divai mpya lazima iwekwe kwa viriba vipya akimaanisha kwamba Yesu ni ujio wa zama mpya na hivyo lazima apokelewe na moyo mpya na roho mpya na si achanganywe na viriba au mioyo ya zamani. Wakifanya hivyo, hawatamuelewa kabisa. Hivyo, Yesu anapaswa aandaliwe nafasi mpya kabisa.
Mfalme Sauli tunayemsikia akikataliwa na Mungu katika somo la kwanza ni kwamba yeye hakuandaa moyo mpya wa kuishi pamoja na Bwana tangu alipo pokea ufalme na ndio maana alishindwa. Yeye alikwenda na viiriba vya zamani. Yeye hakujua kwamba baaada ya kupokea upako na kuwa mfalme, angepaswa abadilike lakini yeye alindelea na moyo ule ule, wa kukosa utii, tamaa, kuweka maslahi mble na ndio maana alishindwa. Hivyo ndugu zangu tujapo mbele ya Yesu twende kwake na viriba vipya, moyo mpya. Usiende kwake na moyo wa chuki, magomvi na ndugu, moyo wa kisasi, majivuno, au moyo wa kutokutubu, au kutokuamini au ushirikina. Vyote hivi vitoe ili umpokee Bwana. Nenda na kiriba kipya mbele ya Bwana.
©️ Pd. Prosper Kessy OFMCap.