Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la misa takatifu kwa asubuhi ya leo. Leo tunaadhimisha kumbukumbu ya Mt. Sesilia. Leo neno la Bwana katika asubuhi yetu hii linaongozwa na maneno ya wimbo wa katikati: Bwana utukufu wako utakapofunuliwa, furaha yangu itakamilika. Maneno haya yanatuunganisha vizuri na kile tunachokisikia katika somo la kwanza ambacho chanzo chake tulikisikia katika somo la kwanza tulilosoma Jumatatu. Antiochus Epiphanes anataka kuiangamiza dini ya Kiyahudi, anataka Wayahudi waache tamaduni zao walizoamriwa na Musa wafuate taratibu za watu wa mataifa, waachane kabisa na Torati wafuate mambo ya mataifa.
Wanapoamrishwa kula nyama ya nguruwe nao wanakataa-hii kukataa kula nyama ya nguruwe ni picha tu ya kwamba walikuwa wako tayari kupinga chembe yoyote ile ya tamaduni ya watu wa mataifa ili waitetee dini yao. Suala la kula nyama ya nguruwe si suala zito sana kiimani lakini wao walijua kwamba japokuwa kiimani sio zito, madhara yake kiimani hasa kwa vizazi vijavyo ni hatari kwa sababu mtu unapoanza kudharau na kutokuzingatia mambo madogo madogo, jua kwamba imani yako nayo inajiandaa kufa. Hivyo, hawa Wayahudi walikuwa tayari kutetea hata hivi vipengele vidogo vya Imani yao ili kuhakikisha kwamba tamaduni za watu wa mataifa, tamaduni za kishetani hazichukui nafasi, hata kama ni nafasi isiyo ya muhimu sana katika mambo yahusuyo Mungu.
Katika injili ya leo tunakutana na mtumwa aliyeona kwamba atii kwa sababu amepewa kidogo, hakuna haja ya kuifanyia kazi talanta yake. Hii ni kidogo sana na hivyo akazembea na mwisho wa siku alipokuja kuulizwa akasema hajazalisha kitu na akajikuta ananyanganywa kile kidogo alichokuwa nacho na kuadhibiwa Zaidi. Aliona kwamba amepewa kidogo akaona aah!-Bwana wangu hatahitaji chochote kutoka hapa na hivyo akaamua kuzembea. Kwa kudharau kwake mambo madogo, alijikuta anapoteza maisha yake yote. Ndivyo ilivyo kwa hii familia tuliyoisikia katika somo la kwanza. Wanajua kwamba kama wataanza kupuuzia mambo madogo madogo kama vyakula, basi Imani yao itamomonyoka na watakao wafuata nyuma watamomonyoka Zaidi kutokana na mfano mbaya.
Haya masomo ni somo kwetu ndugu zangu. Katika imani yetu, usikubali kupuuzia mambo madogo ndugu yangu. Yanaanza kama mzaha lakini mwishowe yanamaliza kila kitu kiimani. Mnaweza kusema tuondoe baadhi ya sala muda ni mrefu mno, lakini mwisho wa siku hata misa itakuja kuwa ngumu kusali.
Kingine ni kwamba mnapofanya hivi, kile kizazi kinachokuja kinakwazika Zaidi, kinalegeza Zaidi, na kuharibu Zaidi kama watu wasiokuwa na mwelekeo-ndivyo ilivyo ndugu zangu. Na tunakosa kuwa mfano kwa vizazi vijavyo. Tusikubali muovu atawale na Kristo akose nafasi maishani mwetu.
Hivyo ndugu zangu, Imani yabidi uwe makini. Usiruhusu kitu kama uvivu katika imani, usiruhusu kulegeza legeza mambo. Ukilegeza sasa, kizazi kijacho kinaua zaidi.
©️ Pd. Prosper Kessy OFMCap.