Mtafute Bwana Mapema
“Ee Mungu, Mungu wangu, nitakutafuta mapema, nafsi yangu yakuonea kiu.” Hii ni Zaburi iliyoimbwa na Daudi akiwa katika jangwa la Yudea kabla ya kuupata ufalme. Kipindi hiki alikuwa akiwindwa na majeshi ya Sauli. Pia kulikuwako na waliokuwa wanapeleka habari za Daudi kwa Sauli. Na pia Daudi alikuwa na rasilimali ndogo sana kwa ajili ya mapigano yake na Sauli. Hivyo alimlilia Mwenyezi Mungu kwa maneno haya.
Wakristo wa mwanzo waliamriwa kuisali Zaburi hii kwa kila siku baada ya kuonekana kwamba maisha yao yalikuwa hatarini kama ya Daudi wakiwindwa na maadui kila mahali. Nasi tusiache kusali. Nafsi za wengi zinaonea kiu vitu kama pombe, vyeo na pesa. Lakini sisi, kama Mt. Augustino anavyotufundisha ni kwamba tuliumbwa kwa ajili ya Bwana, na hivyo hatutatulia isipokuwa katika Bwana. Hivyo, tuombe kutulia katika Bwana.
Katika somo la kwanza, tunapewa sifa za hekima: hungaa bila kufifia, haijivuni na huonekana kwa wanaoitafuta, aitafutaye mapema hana kazi ngumu, humkuta ameketi mlangoni. Hekima ni Mungu mwenyewe: ndiye mwenye sifa za namna hii. Leo jiulize, waweza kuiga sifa za namna hii? Sifa za hekima? Hekima haijivuni na kwa kila anayeitafuta huipata. Wewe jiulize leo-kwa kila anayekutafuta kwa ajili ya msaada anakupata? Unakuwa tayari kutoa msaada wako kwa utulivu wote au msaada wako unautoa pamoja na manyanyaso? Na pia mazungumzo tunayoyafanya kila siku, je, yamejaa hekima ya namna hii? Anayeongea ovyo siku zote ni vigumu kuipata hekima. Jifunze kukaa kimya.
Hekima inaokoa na kuongoza kwenye maisha ya umilele.” Hupatikana kwa kumchagua Bwana Mungu wa Israeli na kuzitii amri zake.
Hekima kwa nyakati zetu inachaguliwa na wachache. Mambo ya kimungu yamepewa nafasi ndogo. Wewe utambue kwamba utachanua kwa kuyapa mambo ya Mungu kipaumbele. Ipe sala kipaumbele. Katika maisha yetu, ipo hatari kubwa endapo tutaiacha imani na maadili yetu na kugeukia mitazamo ya kidunia.
Katika somo la injili, Bwana Yesu anatupa mfano wa harusi wenye kutufundisha namna sisi tupaswavyo kuishi. Harusi ni miongoni mwa matukio yaliyopendwa sana huko Israeli na karamu yake ilifananishwa na ile ya Mwanakondoo kwani kwenye harusi kulikuwa ni furaha tu bila kilio. Wanawali wote walibahatika kupewa mwaliko na Bwana harusi. Lakini baadhi yao walilala usingizi na Bwana harusi alipokuja, walishindwa kumpokea na kumpatia makaribisho stahiki. Hawa wanawali walitumia muda wote kufanya ya kwao tu na kusahau ya Bwana harusi.
Ndivyo ilivyo hadi leo; wengi tumesahau wajibu wetu kwa Mungu. Wanawali wapumbavu walishindwa kulipa heshima tukio la Bwana harusi. Tabia ya kudharau mambo ya msingi ni hatari sana. Maisha ya mkristo ni mkesha akipambana na vilema mbalimbali kama ulevi, uasherati, wizi na kutokusali. Hatujui siku wala saa na hivyo lazima tuishi kinyenyekevu. Wanyenyekevu huvuna mema ya nchi. Wanawali wapumbavu walikuwa wabinafsi wakifikiri ya kwao tu. Nawe leo ubadilike, yape kipaumbele ya Mungu. Muda wa kumsubiri Bwana harusi ni muda tuliopewa kwa ajili ya kuishi. Hivyo, muda huo utumie vizuri kwa kusali, kuomba na kushukuru.
Sala: Bwana tusaidie tushikilie taa zetu za imani zikiwaka daima hivyo tukutane nawe daima, Amina.
------------------------------------------------
©️Pd. Prosper Kessy OFMCap.