Ndugu zangu wapendwa, karibuni kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika asubuhi ya leo tunaanza kwa kuliangalia somo la kwanza. Hapa tunakutana na ujumbe mzuri kabisa kwamba wanaomcha Mungu wako katika mikono salama ingawa kwa wengine wanaonekana kana kwamba imekula kwao, ati kwa sababu hawakuzifurahia raha za dunia, ati kwa sababu walipoteza muda wao kusali, kusaidia maskini, kutoa sadaka kanisani, kuwa na mke mmoja tu. Wanaona kwamba hawakuweza kufurahia hata kidogo na sasa wanakufa hivi hivi bila ya chochote, bila ya miili yao kufurahia chochote hasa wale wanaokufa kijana(Waliokuwa wakiona hivyo ni Maepikureans waliokuwa wakisisitiza watu waponde anasa iwezekanavyo kwani maisha ni hapa duniani tu). Hapa mwandishi anajibu mapigo ya maepikureans waliokuwa huko Alexadria walivyokuwa wanawakejeli Wayahudi Wachamungu. Mwandishi anasema hapa kwamba mambo ni tofauti na maepikureans wanavyofikiria. Wajue kwamba hata wakifa, bado watazidi kuwa katika mikono salama licha ya ukweli kwamba watakuwa wanadhihakiwa na Epicureans. Kuna wakati utafika ambapo watangaa na maepikureans watakuwa wanalia na kusaga meno. Hivyo mwandishi anawaeleza kwamba wazidi kubakia katika kumtegemea Mungu na wasiyumbishwe na maepikureans.
Ujumbe huu wa somo la kwanza unaendelezwa vizuri katika injili Yesu anapowaambia wanafunzi wake kwamba baada ya kufanya utume wao, waseme sisi ni watumwa tusio na faida, tumefanya tu kile tulichopaswa kufanya kwa kweli hili lilikuwa jambo la muhimu sana katika maisha yao ya kitume. Na ulikuwa ni ujumbe mkubwa sana kwao. Tulisikia Yesu akitoa maneno yanayofanana na haya muda mfupi kabla ya kifo chake. Yesu alimwambia Baba hivyo hivyo katika Yohane 17:4 kwamba ile kazi uliyonituma kutenda nimeimaliza Baba. Mtakatifu Francisko wa Assis mwenyewe alitamka hili kwa ndugu zake muda mfupi tu kabla hajafa , kwamba "nimefanya yangu, naomba Mungu awasaidie muweze kutimiza ya kwenu". Maneno haya yalisemwa ili wanafunzi wake wajue kwamba kazi yao ya injili ipo mikononi mwa Mungu na wamtegemee Mungu aiongoze na si sifa au tuzo yoyote toka kwa mwanadamu bali toka kwa Mungu na Mungu ndiye anayeipima, haipimwi kwa vigezo vya mwanadamu hata siku moja. Hivyo, wasiache kumtegemea Mungu katika utume wao na ikitokea kwamba watu wamekataa kuwakubali, wasishtuke kwani kazi yao haitegemei vigezo toka kwa binadamu.
Hapa tunayomengi ya kujifunza ndugu zangu: nakwambia pale kanisa au mkristo yeyote alipopokea sifa za watu na kuvimba kichwa waliishia katika madhara makubwa. Kanisa la sardis katika ufunuo 3 lilianguka kwa sababu lilikubali kupokea sana sifa za binadamu, likafanya kazi kadiri ya matakwa na mapenzi ya mwanadamu na mwishowe likaja kuitwa na Yesu kama kanisa mfu. Hata wewe ndugu yangu ukijidai kupokea pokea sifa za watu bila kujiuliza ukweli wa hizo sifa na wewe ukajidai kuzipokea na mwishowe ukatenda kadiri ya watu wanavyotaka nakwambia utaishia kuwa mfu vilevile. Katika kila sifa unayopokea chunguza namna ambavyo yaweza kuwa chanzo cha wewe kupotea kiroho. Hili ni muhimu ndugu zangu sana.
Kingine ni kwamba tusishtushwe ndugu zangu tukiona baaadhi ya watu wanatukejeli juu ya msimamo wa kiimani, kwa nini wewe unaenda jumuiya na wewe ni mheshimiwa hivyo, kwa nini unakuja na kukaa kwenye mkeka ili kusali jumuiya kwa mwenzako-nakwambia ndugu yangu usishtushwe au kuteswa na haya. Watakatifu wengi walinyanyaswa hivyo hivyo, mti wenye matunda mazuri hupigwa mawe ya kutosha. Hivyo, tubaki imara siku zote. Lakini na wewe unayemtukana na kumkejeli mwenzako kama wale Epicureans wa somo la kwanza uangalie vizuri kwa sababu kuna wakati watakuwa wanacheka wale uliowatesa na wewe utakuwa unaumia.
©️ Pd. Prosper Kessy OFMCap.