Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la misa Takatifu. Bado tupo katika kipindi cha majilio na neno la Bwana linaanza kwa kuliangalia somo la kwanza. Hapa tunamkuta nabii Isaya akitabiri ujio wa nyakati za Kimasiha ambapo tunaelezwa kwamba huyu Masiha atakuwa mfalme wa ajabu, kiumbe ambacho kwa uwepo wake tu ni kama vile dunia inapata mwamko mpya. Yaani tunaelezwa kwamba kutakuwa na Amani ya ajabu duniani. Na Amani hii itafikia hadi kwa viumbe. Hata simba atadiriki kula majani ili asidhuru kiumbe kingine-mtoto mdogo atacheza pembeni mwa shimo la nyoka. Yaaani hakutakuwa na uadui wowote kabisa.
Ndugu zangu, Yesu alipokuja duniani kwa mara ya kwanza, kwa wale waliompokea, hili lilifanikishwa kwao. Hizi zama za Kimasiha ziliweza kutokea. Yaani uadui ulikoma kwa wale waliompokea, watoza ushuru kama akina Zakayo waliweza kuanza maisha mapya, makahaba nao waliweza kukaribishwa kwa Yesu na kuanza maisha mapya, uadui uliokuwako kati ya Wasamaria na Wayahudi ulikomeshwa. Nakwambia na hadi sasa, wale wote waliopokea mafundisho ya Yesu wameishia kuishi katika Amani ya ajabu.
Lakini kama tunavyosikia katika injili ya leo, mambo haya yalitokea tu kwa wale walioonekana kama watoto wachanga. Wale ambao walijishusha na kuyapokea mafundisho haya, na kumfuata Yesu. Lakini waliokuwa wanajivuna, nakwambia hakuna lolote lililowezekana kwao. Walifikia kiwango cha kumwona Yesu kama adui yao na kumwona Yesu kama mleta vurugu, aliyekuja kuporomosha ulaji wao.
Ndugu zangu, Yesu ambaye alipokuja kwa mara ya kwanza aliweza kuleta Amani ya ajabu hasa kwa wale waliopokea mafundisho yake, nasi tutambue kwamba atakapokuja kwa mara ya pili, atakamilisha vizuri Zaidi kile alichoanza. Sisi tunaosubiria ujio wa pili wa Yesu tuzidi kumpokea Yesu. Tuendelee kuhudhuria ibada zake zote, kuabudu zake zote, kupokea sakramenti zake zote na kubakia katika kanisa la Kristo.
Tuzidi pia kuwapenda wenzetu, kuwasambazia Amani, Amani iwafikie hata na wao pia. Wafurahi namna jinsi Yesu alivyoweza kusambaza Amani hadi kwa viumbe. Nasi tuache kuwafanya baadhi ya ndugu zetu kuishi maisha magumu kutokana na ukorofi wetu. Msiwaonee wake zenu, kuwapiga au kuwatendea unyama, wala mke usimtende mumeo vibaya. Tuvipelekee viumbe vyote Amani. Tuache hata kuwapiga paka mateke, mbwa unawapiga kwa mawe bila hata sababu. Hata tukikutana na viumbe tusiviue au kuvikanyaga kanyaga. Kuwa mjumbe wa amani.Tuzidi pia kuendelea kupokea sakramenti ya kitubio na hii itatufanya tuzaliwe upya.
©Pd. Prosper Kessy OFMCap.