Leo tuna adhimisha sherehe ya Bikira Maria mkingiwa dhambi ya asili. Maria ni Mkingiwa Dhambi ya Asili: Somo la kwanza laelezea jinsi dhambi ya asili ilivyoingia ulimwenguni. Ilisababishwa na ukosefu wa utii wa mwanadamu kwa kula tunda la mti uliokatazwa. Dhambi hii ni chanzo cha kifo, kutokuaminiana, hofu baina ya viumbe pamoja na dhiki. Binadamu wote hurithi dhambi hii mara wanapozaliwa lakini Bikira Maria alikingwa asipate dhambi hii. Mungu mwenyewe ndiye aliyemkinga na dhambi hii ili akawe kikao kitakatifu cha mwanae.
Ukweli huu unadhihirika katika injili ya leo pale malaika anapomsalimia Maria kwa maneno kwamba ni mwingi wa neema. Hii yamaanisha kukosekana kwa doa lolote la dhambi kwa Bikira Maria na mtoto atakayemzaa hatakuwa pia na doa lolote la dhambi. Miili ya wote wawili, Mama na mtoto haikuoza kaburini. Yesu alipaa mbinguni mwili na Roho na Maria alipalizwa mbinguni mwili na Roho (Katekisimu ya Kanisa Katoliki 966). Hivyo, tusiogope kuomba kupitia maombi ya Mama Maria sisi tuliozaliwa na dhambi ya asili. Yeye aliiletea dunia neema. Yeye atatugawia neema alizopewa na Mungu na pia atatupeleka kwa Yesu mwanae. Yeye ndiye aliyekuwa hewa kw Yesu alipokuwa tumboni kwake, alikuwa miguu ya Yesu pia alipokuwa tumboni mwake. Yesu alitwa mwili katika mwili wa mama huyu. Kamwe huwezi kusema unampenda mtoto nakumkataa Mama yake. Ukinipenda mimi alafu ukamchukia Mama yangu siwezi kukufurahia.
Tumwombe tukisema, Ee Maria uliyekingiwa dhambi ya Asili utuombee sisi tunaozaliwa na dhambi ya Asili! Amina!.
©️Pd. Prosper Kessy OFMCap