Yesu ni Mfalme anayeishi katika wenzangu
Kristo ni Mfalme na kanisa linatambua kwamba mwanzilishi wake ni mfalme. Mfalme ni mtu mwenye madaraka, anastahili sifa na heshima. Sisi tutambue kwamba tutapaswa kutoa hesabu yetu kwa Yesu aliye mfalme wetu siku ya mwisho. Leo tutafakari namna tutakavyopeleka ripoti nzuri kwa Yesu juu ya uhusiano wangu na wenzangu wanaonizunguka. Katika somo la injili, Bwana Yesu amedhihirisha kuwa yeye ni Mfalme. Ametangaza kwamba katika siku za mwisho atatokea katika utukufu mkubwa na viti vya hukumu vitawekwa. Kwa kipindi hiki ufalme wote wa mwanadamu utakuwa umetoweka na hakuna kitakachokuwa kimesalia.
Na Bwana Yesu atakaa katika kiti cha hukumu ambapo kondoo watabaguliwa na kutengwa na mbuzi. Kondoo ni ishara ya mfuasi mwema na mtiifu. Mbuzi ni ishara ya ukaidi. Mbuzi ni ishara ya wanadamu wenye kujiamulia maisha yao wenyewe na kushindwa kumpatia Bwana Yesu nafasi bora katika maisha yao. Sisi tutambue kwamba maisha yetu ni kuepuka tabia za mbuzimbuzi. Tunapaswa tukubali kutawalika na mchungaji Bwana wetu Yesu Kristo. Tutawaliwe na mafundisho yake, tutawaliwe pia na viongozi aliowachagua hapa ulimwenguni. Katika hukumu hii, kigezo kinachotumika ni uhusiano kati ya wanadamu na wanadamu. Namna walivyohudumiwa wale wenye mahitaji.
Yesu anajidhihirisha kwamba yupo katika wale wadogo tunaokutana nao. Hili lilikuwa jambo geni kwa wengi. Hata wale wenye dhambi walisema kwamba hakika wangalikuwa tayari kutoa msaada endapo kama ni Yesu angekuja kwao katika sura yake mwenyewe. Yesu anataka tuishi kwa uhuru. Na matendo anayoyaangalia sana ni yale tunayotenda tukiwa katika uhuru kamili, bila kusukumwa na watu. Haya ndiyo yanayookoa. Yesu siku zote ni Mungu wa surprise. Hata ujio wake ni wa surprise. Hivyo, tunapoendelea na shughuli za maisha yetu, tufanye tukitambua kwamba tutafanyiwa surprise siku moja.
Nabii Ezekiel anasema katika somo la kwanza kwamba Mwenyezi Mungu atakuwa mchungaji kwa kundi lake. Huu ni uchungaji wenye huruma, wenye kujali walio wagonjwa, na wahitaji. Wengi kati ya wachungaji tuna tabia ya kujijali sisi wenyewe tu kwanza. Mchungaji anapaswa ajue kwamba yeye ni mtumishi. Papa ni mtumishi wa watumishi wa Mungu. Nabii anatangaza kuwaharibu wale kondoo wanono. Kondoo wanono wanayo tabia ya kuwaonea wengine. Na walipata unono wao kwa kudhulumu wenzao.
Tunaalikwa tuwapatie maskini kipaumbele. Mwishowe kila kitu kitawekwa chini ya Yesu atakapotoa hukumu. Tuisubirie hukumu hiyo katika matumaini yote na kwa mioyo misafi na mitukufu.
Sala:
Bwana, wewe ni mfalme wa ulimwengu. Njoo utawale maisha yangu na ufanye moyo wangu kuwa sehemu yako ya kuishi, Amina.
©️Pd. Prosper Kessy OFMCap.