Ujumbe: Sawazisha milima na mabonde ili Kristo aanzishe yote upya
Ndugu zangu, kuna adha kubwa ukutanapo na bonde au mlima katika safari yako. Mlima na mabonde hurefusha safari, hutufanya tutumie muda na nguvu nyingi lakini kaeneo unachotembea ni kafupi sana. Na gari la kawaida likitumika mabondeni au milimani, huchakaa mapema zaidi.
Kingine ni kwamba watu wa milimani au mabondeni wanaonekana kama wako nyuma ya wakati, washamba na hawavijui vitu vya kisasa. Na shuleni walidharaulika, na kama kulikuwa na Tv au redio wewe wakutoka milimani au mabondeni uiguse halafu iache kuonyesha, unadharaulika. Wakikuona na nguo mpya au T-shirt zile za wachezaji umevaa wanakuuliza umepata wapi? Wanafikiri hata baiskeli hujui kuendesha. Na kwa wale wanafunzi hasa wa form one hivi, kama unatokea milimani au mabondeni ukiongea hawakusikilizi. Huna jipya, hata Kiswahili hujui. Bondeni utatuletea habari za kufuga ngombe tu. Hata waalimu walidharau na siku ya mikate watakuangalia unavyotumia jam
Ndugu zangu, kama hawa walidharaulika hivi, naamini walio na milima au mabonde moyoni mwao, hudharaulika zaidi. Hawa watadharaulika si tu na wanafunzi hata na wale wasio wanafunzi.
Katika somo la kwanza tunamkuta nabii akianza kwa kuwapatia wana wa Yuda matumaini. Anaanza kwa kuwatuliza mioyo kuonyesha kwamba walikuwa katika maumivu mazito. Wanaambiwa adhabu yao imefikia mwisho na sasa waupokee msamaha wa Mungu. Wanaelekezwa kutengeneza njia kwa ajili ya Bwana anayekuja kuwatembelea huko utumwani. Wasawazishe milima na mabonde yote ili awafikie kwa haraka.
Nabii anaendelea kutoa matumaini makubwa na sehemu ya pili ya somo anawageukia Wayahudi waliosalia Yerusalem ndani ya ule mji wa magofu, wazee na viwete na maskini. Wajumbe wao wanaelekezwa kupaaza sauti zao kwa nguvu na kuwapatia matumaini kwamba Bwana anakuja Yerusalem akiambatana na lile kundi la wenzao waliokuwa utumwani na huko atalilisha kundi lake mwenyewe.
Unabii huu ndugu zangu uliashiria mwanzo mpya kwa taifa hili la Yuda; ujio wa Bwana kati yao kuwakomboa. Wangeendelea kubakia kule Babuloni, Imani yao ingekwisha na wangepotea kama taifa. Hivyo, sasa iliwabidi wamwandalie wamkaribishe aingie kwao kwa furaha awaletee ukombozi. Picha hii ya kuandaa njia ilichukuliwa na nabii toka kwa wale wafalme na makaisari wa zamani. Kabla ya ujio wao ilibidi kuwaandalia njia, unafukia mashimo na mabonde ili magari yao yapite vizuri. Hata kwa maeneo fulani, Askofu au pmPadre mpya anapokwenda nyumbani, wanakijiji wanakuandalia njia.
Ndugu zangu, mwaka 539BC Bwana aliweza kufika kwao huko Babuloni na kulikomboa taifa hili. Lakini cha ajabu kuna Wayahudi waliokataa kurudi au kuandaa njia, walioona ujumbe huu kuwa shida kwao na kukumbatia mashamba yao, na taratibu hawa walifunikwa na mataifa mengine na kupoteza Uyahudi wao.
Katika injili, tunakutana na mwendelezo wa hii mada ya kutengeneza njia ya kwa ajili ya mfalme mwingine aliyetegemewa. Na yaonyesha kwamba huyu alikuwa mfalme mkuu sana na dunia ilikuwa ikijiandaa kwa ujio mkubwa sana. Yohane Mbatizaji leo anatueleza kwamba Huyu alikuja kuwabatiza watu kwa Roho na moto, anakuja kutukomboa na lile kosa lililofanywa na wazazi wetu, kutufungulia neema, kumpatia mwanadamu Roho Mtakatifu atakayesafiri nao kama mtoto wa Mungu, na kuwafikisha kwa mbinguni.
Hii ni habari njema mno na Yohane anatumwa kuwaandaa watu, si kwa kuchimba njia kama walivyofanyiwa makaisari bali kwa kuwaandaa kiroho, kuwabatiza kama ishara ya nje kwamba wametubu ili zama za huyu mfalme zipenye nyoyoni mwao. Na Yohane Mbatizaji alijitolea nguvu zake zote kuutangaza ujio wake ili lawama isiwe kwake. Alivaa ukanda wa ngozi ya singa na kula nzige na asali.
Yaani, alidiriki hata kutotumia nguo au chakula kizalishwacho na jamii, na kula chakula cha mwituni, nzige na asali na kuvaa mavazi ya wanyama kuonyesha kwamba jamii ninayoiambia itubu iliishi katika dhambi na msipotubu sipo tayari kula au kuvaa chochote kizalishwacho na jamii. Na kumbuka kwamba wafarisayo walikuwa wakimtafuta waone vilema vyake, walijiuliza huyu anayetulaumu hivi yeye anaishi je? Yeye anakula na kunywa kitu gani? Anakulaga vitu vya dhuluma? je ni mlevi, ni mlafi? Na waliposhindwa kumkamata walimuita basi ana pepo.
Yote hayo yalifanywa na Yohane kuonyesha kwamba kumpokea Kristo ni kuanzisha mabadiliko ya kimaisha na hivyo ile jamii ilibidi itubu, huwezi kumpokea Kristo bila ya kukubali mabadiliko ya kimaisha na Marko anatumia maneno “mwanzo wa injili ya Yesu Kristo” kumaanisha kwamba Kristo anakuja kuumba vitu upya.
Na anatualika na sisi kuiumba mioyo yetu upya tena na tunaiunda kwa kusawazisha mabonde na milima yanayotufanya tushindwe kumfikia Mungu, kumfanya Mungu atumie muda mrefu kukufikia kama baadhi ya wale Wayahudi wa somo la kwanza waliokataa kurudi.
Vitu kama kushindwa kuona mahitaji na mateso ya wengine- unakutana na mtu anayetembea kama anataka kuanguka na wewe hujali, mtu anakulilia sijala tangu jana wewe hujali, unasema huyu ni mhuni, mwizi tu; yote haya ni mabonde na milima yanayotuzuia kumfikia kristo.
Kingine ni mpangilio mbaya wa matumizi bila kujali wengine-uko tayari kumwagilia ukoka maji lakini wenzako hawana maji, uko tayari kununua nguo ya gharama, simu kubwa, na pesa za kwenda bar kila wikiendi lakini wazazi wako kijijini wanakufa njaa au ni wagonjwa au hujamlipia ada mtoto. Unahangaika kununua perfume, sabuni za bei ili watu wakusifie lakini madeni hulipi na unamtesa mwenye nyumba kila mwisho wa mwezi. Uko tayari kumwaga chakula au kumpatia mbwa kuliko kumpatia jirani yako hapo. Familia moja ya kijiji Fulani ilikuwa na tabia ya kukaa na mchele au mikate hadi inaoza. Waliona afadhali kutupa kuliko kuwapa wengine. Matumizi ya pesa ya mtindo wa kibinafsi namna hii ni wa kishetani. Unaacha wenzako wanakufa bila kujali. Au mgonjwa yuko hapo lakini hutatoa gari yako. Au kila mwaka unanunua nguo lakini bado umelimbikiza hadi zile ambazo ni za fashion ya miaka kumi iliyopita.
Kingine usile vya watu, kula vya kwako ili mtu asikushike kirahisi na ndio maana wafarisayo walishindwa kumkamata Yohane Mbatizaji. Hii ni milima inayobidi kusawazishwa kipindi hiki.
Ndugu zangu, katika somo la pili, tunasikia juu ya Mt. Petro akiwaeleza wakristo waliofikiria kwamba ujio wa pili wa Yesu umechelewa sana.
Paulo anawaambia kwamba Yesu hajashindwa kurudi. Anasema ujio wa pili wa Kristo si mchezo, si suala tu la kuongea hivi hivi. Tumesikia kwamba akija mbingu zote zinafumuliwa, na viumbe vya asili vitateketea. Na hata nyie mnaweza mkateketea vilevile. Hivyo kukawia kwake kuoneni kama nafasi kwenu ya kutubu na si kuanza kufikiria kwamba hakuna Mungu au Mungu hana nguvu. Tuitumie nafasi hii vizuri.
Jiulize kitu kimoja-kama Kristo angerudi mara, na kuuhukumu ulimwengu na dunia kutoweka na vitu vyote kuteketezwa, labda mimi nisingekuwapo.
Hitimisho: Ndugu zangu, Nilianza kwa kusema kwamba baadhi ya watu wanaposikia wewe umetokea milimani au bondeni, wanakudharau. Lakini nakwambia aliyebeba milima na mabonde moyoni hudharaulika Zaidi.
We niambie-mtoto wako akikuona unamkimbia mama anayekuja kuchukua kodi ya nyumba halafu unamwambia akija mwambie sipo, huyo mtoto atakuonaje, na watoto wa majirani watakuonaje? Au mtoto akikuona unazunguka round ndefu unamtuma akaombe chumvi kwa jirani aliyeko kilometa kumi na kumwacha huyo wa pembeni kwani mmekosana naye, sasa huyo mtoto atakufikiriaje? Au hata vijana wakisikia kwamba wewe unaishi kwa madeni tu au una simu kubwa lakini ni kukopa tu, nakwambia hawatakuheshimu. Watawaheshimu wale wa kutoka milimani kuliko wewe.
Kristo alishakuja kwa mara ya kwanza. Tunaposubiria ujio wake wa pili, tusawazishe mabonde na milima hasa ya kutowajali watu. Namna njema ya kujiandaa ni kutumia sakramenti ya upatanisho na kuwaomba msamaha wenzetu, hii hufukia mabonde yote na kumfanya kristo atufikie kirahisi.
Halafu tusiwasahau wenzetu, hasa wale wenye shida. Unapofadhili unapata mwombezi na Bwana atakufikia kirahisi. Tumsifu Yesu kristo.
©️Pd. Prosper Kessy OFMCap.