Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika asubuhi ya leo tunaanza kwa kuliangalia somo la kwanza. Hapa tunaona sasa Wayahudi wamechukizwa kabisa na madhulumu, maonevu ya Wagiriki. Wanakasirika kuona wakidhalilishwa kama mbwa, kuona ati watu wanakuja na kuwalazimisha waiache dini yao, waiache imani yao, na kuona jinsi baadhi ya Wayahudi wanavyoogopa na kudiriki kuiacha imani yao na kama ilivyo kwa yule wa somo la kwanza leo baadhi ya Wayahudi walilazimishwa wakakubali ati watolee sadaka kwa miungu na kuacha imani yao.
Sasa leo kiongozi wa Wayahudi aitwaye Matatiasi anakataa huu udhalilishaji na anaamua kuanzisha mapambano dhidi yake na tukisoma katika hiki kitabu zaidi tutaona kwamba mapambano yaliyoongozwa na Wayahudi dhidi ya Wagiriki yalifanikiwa. Wayahudi walishinda na katika somo la Jumamosi tutaona jinsi huyu kiongozi wa Kigiriki aliyekuwa anaongoza huu uonevu na udhalilishaji atakavyoshindwa vibaya. Hivyo, ndugu zangu, kwa kumtetea Mungu, wanashinda.
Lakini katika injili tutakutana na kitu tofauti kabisa. Yesu anaulalamikia mji, mji uliokataa kumtetea Mungu, mji ulikataa kumheshimu Mungu, mji uliokataa kumpokea Yesu na mafundisho yake. Yesu anaulilia na kusema kwamba utaangukia pua. Na kweli ndugu zangu, mji huu uliangukia pua kwani mwaka wa 70AD kulitokea Warumi waliokuja na kuuteketeza mji huu kabisa kabisa na hii ilitokana na ukaidi wao wa kutokumtii Mungu, kungangania maslahi yao na hivyo mwishowe walishindwa.
Hili liwe fundisho kwetu ndugu zangu. Kasirikia kuona uovu ukitawala, kuona muovu anataka kurudi na kupata mamlaka ya kutawala tena. Kasirika kama matatiasi alivyokasirika. Ukipita ukisikia watoto wakitukana, waonye. Usikae kimya ndugu yangu. Ukiona kuna mtu anamnyanyasa mwenzake-saidia. Usiwe kama wale Mafarisayo wa Yerusalemu walivyojiunga nao kutenda maovu mwishowe wote wa Yerusalem waliangukia pabaya. Kuwa kama matatiasi. Yeye alishinda.
Na wewe usijiunge na muovu kumkandamiza mwema hata siku moja, nakwambia kuna siku moja utaangukia pua tu. Hivyo, mtu mwema huwa hashindwi hata kidogo. Atakushinda tu kama wewe utajipeleka kwa ubaya.
Kingine ni kwamba ukimtetea Mungu mbele za watu huwa hakuachi hata kidogo. Atakutetea tu. Angalia hawa wa somo la kwanza. Walianzisha mapambano kuliko kukubali waache imani yao. Na jumamosi tutasikia jinsi walivyoshinda na huyu kiongozi aitwaye Antiokus Epiphanes alishindwa vibaya ajabu. Nasi tusiogope kumtumikia Mungu ndugu zangu. Tupambane kwa ajili yake nasi tutashinda tu.
©️Pd. Prosper Kessy OFMCap.